Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yapanga kuongeza kodi mafuta ya kula yanayoingia nchini

Alizeti Pic Serikali yapanga kuongeza kodi mafuta ya kula yanayoingia nchini

Mon, 29 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wizara ya Kilimo inafanya mazungumzo na Wizara ya Fedha na Mipango kuangalia kuongeza kodi kwa mafuta yanayoagizwa nje ya nchi ili kukabiliana na kuporomoka kwa bei ya mafuta nchini.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Mei 29, 2023 na Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Meatu (CCM) Leah Komanya.

Mbunge huyo alitaka kujua kauli ya Serikali kuhusu kuporomoka kwa bei ya alizeti kwa zaidi ya asilimia 50 wakati nchi ina hali inaupungufu mkubwa wa kutosheleza kwa mafuta ya kula.

Akijibu swali hilo, Mavunde amekiri kuwa bei ya alizeti imeporomoka na kusababisha kuwakatisha tamaa wakulima.

“Lakini sisi tumekaa na Wizara ya Fedha na Mipango na kuangalia namna bora ya kutatua changamoto ikiwemo kuangalia sera zetu za fedha na hasa katika kuboresha eneo la kuongeza kodi kwa mafuta ambayo yanaagizwa nje nchi ili kuwalinda wakulima wetu,”amesema.

Naye Mbunge wa Kiteto (CCM), Edward Lekaita alihoji wakati wanaangalia kuhusu uongezaji wa kodi kwa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi kwanini isichukue hatua ya kununua mazao yote.

Akijibu swali hilo, Mavunde amesema ni kweli wamepata changamoto na ndio maana katika bajeti iliyopita walieleza juu ya kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya kilimo ambayo huko baadaye wanaweza kufanya kazi ya kusawazisha (stabilization) bei inapotokea masuala kama hayo.

Katika swali la msingi Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mwantumu Dau Haji amehoji Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya bei ndogo kwa mazao pamoja na ukosefu wa masoko ya uhakika nchini.

Akijibu swali hilo, Mavunde amesema Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wakulima wanapata bei shindani na masoko ya uhakika.

“Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza tija kwenye uzalishaji kupitia uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji, pembejeo, utafiti, huduma za ugani, matumizi teknolojia na kurasimisha Sekta ya Kilimo mazao,”amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live