ZANZIBAR; KAMPUNI ya mwani inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ya Zasco imeanza kununua zao hilo kwa wakulima na bei imepanda kutoka Sh 600 hadi Sh 1,000 kwa kilo.
Waziri wa Uvuvi na Uchumi wa Buluu, Suleiman Masoud Makame amewaeleza wajumbe Baraza la Wawakilishi kwamba hayo ni matokeo ya ubunifu wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kuunda kampuni ya kununua zao hilo.
Makame alisema lengo la SMZ kuunda kampuni ya mwani ni kuunga mkono juhudi za wakulima ambao kwa asilimia 80 ni wanawake.
Alisema juhudi hizo zinakwenda sambamba na ujenzi wa kiwanda cha kusarifu na kuongeza thamani ya zao la mwani kuongeza uzalishaji wa bidhaa ili kufikia malengo na mahitaji ya kiwanda yaliopo ya uzalishaji wa tani za mwani 30,000 kwa mwaka.