Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaondoa kodi kwa vifaa tiba corona

WAZIRI MPANGO Serikali yaondoa kodi kwa vifaa tiba corona

Mon, 4 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SERIKALI imeondoa kodi kwenye vifaa tiba vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi, ili kurahisisha upatikanaji wake katika kukabiliana na maambukizo ya virusi vya corona.

Pia, imeahirisha matumizi ya baadhi ya fedha zilizokuwa zimeshapangwa ikiwamo kusitisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo haijaanza kabisa na fedha hizo kuelekezwa kupambana na corona.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliyasema hayo bungeni juzi jijini Dodoma.

Alisema Aprili 16, mwaka huu, Waziri wa Afya alipeleka orodha ya vifaa 15 vya nyongeza vinavyostahili kusamehewa kodi kwa ajili ya kupambana na corona.

“Tulishatoa ridhaa na vifaa vyote hivi vitaingia nchini bila kulipiwa ushuru wa forodha, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), lakini tumeweka masharti kidogo ili msamaha huo usitumike vibaya,”alisema.

Kwa mujibu wa waziri huyo, wamechambua mafungu mbalimbali ambayo matumizi yake yanaweza kuahirishwa ili kuelekeza fedha zake kwenye matumizi ya dharura na kuongeza kasi ya kulipa malimbikizo ya makandarasi, watoa huduma na watumishi ili kuhakikisha fedha zinawafikia.

Alisema kipaumbele ni kukinga watoa huduma za afya na wananchi na kwamba kwa kipindi cha Machi hadi Septemba mwaka huu, zinahitajika Sh. bilioni 382.5 kwa ajili ya kukabiliana na corona.

“Mpaka sasa, tumekwishatoa Sh. bilioni 15.49 kwa Bara na Sh. milioni 500 Zanzibar. Tunagharamia upatikanaji wa mahitaji ya msingi ambayo ni pamoja na vifaa vya kujikinga na kuwakinga watoa huduma, dawa, vifaa tiba, vitendanishi na kuongeza mashine za kupumulia, magari ya kubebea wagonjwa na kuimarisha kambi zilizopo.

"Tumeendelea kuhimiza sekta binafsi kuchangia mfuko wa maafa na hadi sasa zimepokewa Sh. bilioni 1.945 zilizoelekezwa kwenye vifaa vya kujikinga na inapunguza mzigo kwa serikali. Tunaomba fedha kutoka Shirika la Fedha Ulimwenguni zenye riba sifuri na masharti nafuu na tunatarajia kupata majibu," alisema.

Alisema kuwa juzi alipokea barua kutoka Benki ya Dunia (WB) ambao wamesema huenda wakasimamisha madeni kuanzia jana (Mei Mosi) hadi Desemba 31 mwaka huu.

“Tunafanya jitihada kubwa timu ya kitaaluma inachambua taarifa za kila sekta, kuangalia athari ni nini na nini kifanyike ili tukabiliane na corona. Hizi za kisekta zinahitaji uamuzi wa jumla wa serikali kama kuahirisha matumizi ya baadhi ya maeneo na kuna miradi ya maendeleo ambayo haijaanza kabisa,” alifafanua.

Waziri Mpango alisema wanatarajia kutoa unafuu wa kodi kwa biashara ambazo zitaathirika na kurefusha muda wa marejesho ya mikopo na kuipitia upya ili kuwasaidia Watanzania.

“Serikali inakamilisha mkakati mahususi na utapitishwa kwenye ngazi mbalimbali za maamuzi serikalini. Tunataka Watanzania wajue serikali inajali watu wake na ipo makini kwa jambo kumbwa kama hili la kuokoa nguvu kazi ya taifa,” alisema.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema motisha kwa watumishi imeanza kwa baadhi ya halmashauri kutenga hosteli kwa watumishi wanaotoa huduma wakae kwa siku 14 kabla ya kuungana na familia zao.

“Corona itakuwapo, lazima tujifunze kuishi nayo kwa kuchukua tahadhari na ndiyo maana tunatoa elimu kwa namna mbalimbali, pia kutumia tiba asili na tiba mbadala,” alisema.

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Faustine Ndugulile, alisema upotoshaji umekuwa mkubwa kutokana na watu wengi kujigeuza wasemaji na madaktari, akitaka wataalamu kuachwa kufanya kazi ili kupunguza taharuki katika jamii.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live