Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yakwaa kisiki kesi ya kuhoji mamlaka ya Zanzibar kwenye bandari

Bandari Zanzibar Kisiki.png Serikali yakwaa kisiki kesi ya kuhoji mamlaka ya Zanzibar kwenye bandari

Tue, 12 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu imelitupilia mbali pingamizi la awali lililokuwa limewasilishwa na Serikali katika kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na Odero Charles Odero, akihoji shughuli za bandari Zanzibar kuendeshwa na chombo kisicho cha muungano.

Katika kesi hiyo namba 15 ya 2023 iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania masjala ya Dar es Salaam, Odero amemshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na AG wa Zanzibar ameunganishwa katika shauri hilo kama “mdau muhimu”.

Odero anahoji sababu za kikatiba kwa nini uendeshaji wa shughuli za bandari Zanzibar hauendeshwi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kama Katiba ya Tanzania ya 1977 inavyotaka.

Hivyo, anaiomba mahakama itamke na kutangaza kuwa shughuli zote za bandari zilizoanzishwa upande wa Tanzania Zanzibar zinapaswa kuangukia katika mamlaka ya kipekee ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Odero anaiomba pia mahakama hiyo itangaze kuwa TPA ndio chombo sahihi cha Muungano cha kusimamia na kuendesha shughuli zote za bandari Zanzibar, hata zile zilizotajwa na sheria iliyoanzisha Shirika la Bandari Zanzibar ya mwaka 1997.

Mbali na maombi hayo, anaiomba Mahakama itamke kuwa kutungwa kwa sheria ya Shirika la Bandari Zanzibar ya mwaka 1997, kunakiuka Ibara ya 64 (3) na (4) za Katiba na kwamba chini ya Ibara hizo, sheria hiyo ya Zanzibar ni batili.

Odero anaiomba Mahakama imwelekeze AG kuchukua hatua za haraka za kisheria, za kuchukua kwa haraka uendeshaji wa shughuli zote za bandari upande wa Zanzibar na kuziweka chini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TPA.

Kufuatia maombi hayo, Serikali zote mbili kupitia wanasheria wake wakuu, ziliweka pingamizi zikitaka shauri hilo litupiliwe mbali, kwa sababu tatu zinazofanana maudhui, na nyingine iliyoongezwa na AG wa Zanzibar kuwa “ombi hili ni baya kisheria kwa kumshirikisha Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kama mdaiwa muhimu”.

Mapingamizi mengine

Hata hivyo, AG Muungano na AG Zanzibar katika kiapo cha kupinga shauri hilo, walidai kuwa Mahakama Kuu haikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na pili Odero hana nguvu ya kisheria kufungua maombi hayo na katika sababu yao ya tatu, walidai shauri hilo halina maana na limepitwa na wakati.

Wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang’a kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Said Salim Said kutoka ofisi ya AG Zanzibar ndio walifanya wasilisho kutetea pingamizi hilo wakati Wakili John Seka aliwasilisha hoja kupinga pingamizi hilo kwa niaba ya Odero.

Katika wasilisho lao, mawakili wa Serikali walisema kwa kuwa Odero anapinga sheria iliyoanzisha Shirika la Bandari Zanzibar ambacho si chombo cha Muungano kwa mujibu wa Katiba ibara ya 64(3)(4) na (5), Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Walijenga hoja kuwa, kwa kuegemea ibara ya 108 (2) ya Katiba ya Tanzania, muombaji anamaanisha kuwa hakuna jukwaa wala utaratibu wa kushughulikia mambo ya Muungano, wakati chombo kipo kupitia ibara ya 125 ya Katiba.

Mawakili hao walisema kwa maoni yao, Mahakama Maalumu ya Katiba ndiyo chombo sahihi cha kushughulikia malalamiko ya Odero na si Mahakama Kuu.

Pia walisema hawaoni Mahakama hiyo ikipewa mamalaka ya kutafsiri na kubatilisha sheria zilizotungwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kulingana na hoja zao, mamlaka hayo ya kipekee yamewekwa chini ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia Mahakama Kuu ya Zanzibar na ili mahakama iwe na mamlaka hiyo, ni lazima sheria hizo ziwe zinatumika pande zote za Muungano.

Kuhusu hoja ya Odero kutokuwa na mamlaka ya kisheria ya kufungua maombi, mawakili wa Serikali walisema hakuna haki zake zozote zilizokiukwa hadi kufanya akimbilie mahakamani kuomba itoe amri anazoziomba.

Wakijenga hoja kuhusu shauri hilo kupitwa na wakati, mawakili hao walidai kwa kuwa shauri ilifunguliwa chini ya ibara ya 108(2) ya Katiba, linakuwa ni shauri la kawaida la madai, ambalo lilipaswa lifunguliwe kwa kuegemea kanuni za kesi za madai.

Mawakili hao walisema mjadala wa hivi karibuni kuhusu mkataba (IGA) baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai sio ambao unaufahamisha umma kuhusu sheria hiyo ya Zanzibar, bali kama Serikali inataka kuujulisha umma inapitia Tangazo la Serikali.

Mawakili hao walieleza kuwa shauri hilo ni baya kwa kuwa AG Zanzibar ameunganishwa tu kama upande muhimu badala ya kuwa mmoja wa wajibu maombi kamili katika shauri hilo.

Akijibu mapingamizi hayo, Wakili Seka alisema mahakama hiyo ndio chombo pekee chenye mamlaka ya kupokea, kusikiliza na kuamua kuhusu malalamiko ya Odero kupitia shauri hilo namba 15 la 2023 alilolifungua mahakamani hapo.

Wakili huyo alifafanua kuwa pale ambapo Katiba au sheria hazielezi ni chombo gani chenye mamlaka ya kusikiliza jambo fulani, Mahakama ndio yenye jukumu hilo kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuhusu hoja kuwa shauri lilipaswa kupelekwa Mahakama Maalumu ya Katiba, wakili Seka alisema kwa sasa haifanyi kazi na hata kama mteja wake angeweza kuifikia, kutokuwepo kwake kungefanya jitihada zake zisizae matunda.

Alisema Mahakama Kuu ndiyo yenye wajibu wa kusikiliza masuala yoyote ya Muungano kupitia ibara ya 64 ya Katiba ya Tanzania na inaweza kubatilisha sheria yoyote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayokiuka ibara hiyo.

Wakili Seka alisema kukiukwa kwa Ibara ya 64(3) ya Katiba kwa kutungwa kwa sheria hiyo ya Bandari Zanzibar ya mwaka 1997, kunaipa mamlaka Mahakama Kuu kubatilisha sheria kutokana na Baraza la Wawakilishi kupoka mamlaka ambayo si yake.

Uamuzi wa Mahakama

Baada ya kusikiliza mabishayo hayo ya kisheria, Mahakama Kuu ilitoa uamuzi mdogo Machi 4,2024, uliotolewa na Jaji Abdi Kagomba na nakala yake kupatikana Machi 11, kuwa pingamizi hilo la Serikali halina mashiko.

Jaji amesema katika kuamua pingamizi, mahakama itajikita kujibu kama mahakama ina mamlaka kusikiliza kesi hiyo, kama Odero ana mamlaka ya kushtaki, kama shauri limepitwa na wakati na kama si sahihi kumuunganisha AG Zanzibar.

Alisema hakuna ubishi kuwa shauri hilo limefunguliwa chini ya ibara ya 108(2) ya Katiba ya Tanzania sambamba na kifungu namba 2(3) cha matumuzi ya sheria au the judicature and Application of Laws Act, Cap 358 iliyofanyiwa marejeo 2019.

“Ni ibara ya 108(1) iliyoanzisha mahakama hii ambayo inasema mamlaka yake yatatokana na Katiba na sheria nyingine. Inafafanua pale ambapo Katiba au sheria ipo kimya kwa jambo lolote, basi mamlaka hayo yanabebwa na Mahakama”

Jaji amesema “hakuna ubishi shauri lililopo mahakamani limefunguliwa na mtu na si baina ya Serikali mbili chini ya ibara ya 126(1) ya Katiba. Kwa hiyo hoja kuwa shauri lilipaswa kufunguliwa katika Mahakama ya Kikatiba haina msingi”

Jaji amesema kupitia ibara ya 108(2) ya Katiba, mahakama hiyo ina mamlaka yasiyo na kikomo (unlimited jurisdiction) kuhusu masuala ya madai na jinai yanayofikishwa mbele yake, kama shauri hilo lililo mbele ya Mahakama Kuu.

Amenukuu Ibara ya 26 (2) ya Katiba inayosema “Kila mtu anayo haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi zinalindwa,”mwisho wa kunukuu.

Jaji amesema ni mtizamo wa kisheria kuwa mahakama hiyo inayo mamlaka ya kusikiliza mashauri yote ya kikatiba yanayofunguliwa na mwananchi anayepinga kifungu chochote cha sheria, ilimradi tu kuwepo na ukiukwaji wa Katiba.

Akihitimisha uamuzi wake huo, Jaji Kagomba amekubaliana na hoja za wakili Seka kwamba ilikuwa muhimu kumuunganisha AG Zanzibar ili sauti ya Zanzibar isikike na kurutubisha mwenendo na kuwa na amri ya Mahamama ambayo itatekelezeka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live