Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yakiri kutokuandaa Kanzi data ya wajasiriamali

86212 Pic+chalamila Serikali yakiri kutokuandaa Kanzi data ya wajasiriamali

Mon, 18 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKOA wa Mbeya umekiri kuwa haukuandaa kanzi data ya wafanyabiashara wadogo waliopatiwa vitambulisho vya ujasiriamali vilivyotolewa na Rais John Magufuli mwaka jana, hivyo kushindwa kufanya tathmini ya ukuaji wa wafanyabiashara hao.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila, alipokuwa anakabidhiwa vitambulisho vipya 15,000 na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa Mkoa huo, Eunice Mhaluka.

Alisema hali hiyo imesababisha kushindwa kuwabaini wajasiriamali ambao wamekuwa kiuchumi na hawastahili kuendelea kupewa vitambulisho hivyo na badala yake wanatakiwa waingie kwenye mfumo rasmi wa ulipaji kodi unaosimamiwa na TRA.

“Tumeletewa vitambulisho vipya ambavyo tunatakiwa kuviuza kwa wajasiriamali, sasa nawaagiza maofisa biashara wa Halmashauri zote kuandaa kanzi data ya wajasiriamali hawa ili kuwa na utaratibu mzuri wa kufuatilia ukuaji wake,” alisema Chalamila.

Aidha aliwataka wakuu wa wilaya zote kutumia vyombo vyao kuwafuatilia wananchi wote watakaopatiwa vitambulisho, hivyo ili kuwabaini wasiostahili na kuwaondoa kwenye mfumo huo ambao unatoa msamaha wa kodi.

Chalamila aliwataka wakuu wa wilaya kuendelea kuwaelimisha wajasiriamali kuhusu kodi ambazo wamesamehewa kwa mujibu wa vitambulisho hivyo kwa maelezo kuwa baadhi yao wamekuwa wakiutumia msamaha huo vibaya.

Alisema baadhi wamekuwa wakigoma kulipa kodi za nyumba, gharama za kuondoa taka na michango mingine ambayo wanakubaliana katika maeneo yao kitu ambacho alisema sio sahihi.

Akitoa maelezo kuhusu vitambulisho hivyo, Meneja wa TRA Mkoa wa Mbeya, Eunice Mhaluka, alisema mwaka jana mkoa huo ulipatiwa vitambulisho 100,000 lakini mwaka huu vimepunguzwa na kuwa 86,000 ambavyo vitaendelea kuletwa kwa awamu.

Alisema katika awamu ya kwanza walipokea vitambulisho 15,000 ambavyo ndivyo walivyokabidhi, na kwamba wakipokea vingine wataendelea kuvigawa katika Halmashauri zote za Mkoa huo.

Alisisitiza kuwa watahakikisha wanavigawa kwa wajasiriamali wenye sifa pekee ambao ni wenye mauzo ghafi yasiyozidi Sh. 4,000,000, huku akisema kuwa baadhi ya wananchi katika awamu ya kwanza walikuwa wanatafsiri vibaya.

“Vitambulisho hivi vya awamu hii viko tofauti kidogo na vile vya mwaka jana, hivi vya sasa vina namba maalum na haviwezekani kughushi, tunaomba tushirikiane wote kutoa elimu kwa wajasiriamali wetu,” alisema Mhaluka.

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya wa Uchumi na uzalishaji, Said Madito, alisema ili kukabiliana na changamoto zilizojitokeza mwaka jana kwenye vitambulisho hivyo, serikali imetoa utaratibu maalum wa kukabidhi.

Alisema Meneja wa TRA anamsainisha Mkuu wa Mkoa nyaraka maalumu baada ya kumkabidhi na kisha Mkuu wa Mkoa anavikabidhi kwa wakuu wa wilaya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live