Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yakataa kupandisha bei ya mbolea

75016c0c66253d4cc1c25f1dba9ba4e0.jpeg Serikali yakataa kupandisha bei ya mbolea

Sun, 18 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imekataa maombi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ya kuongeza bei elekezi ya mbolea.

Zuio hilo limetolewa juzi na Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda wakati akifungua kikao kazi cha Bodi ya Mamlaka hiyo mjini hapa.

“Bei elekezi ya mbolea sitoongeza licha ya maombi kuletwa wizarani. TFRA nawataka mhakikishe bei ya mbolea iliyopo sasa inaendelea na wakulima wapate mbolea yenye ubora na kwa wakati ili watumie kuzalisha mazao,” alisema Profesa Mkenda.

Profesa Mkenda aliongeza katika agizo lake hilo kuwa ni marufuku kuongeza bei elekezi kwa kuwa lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuona gharama za uzalishaji wa mazao zinashuka ili wakulima waongeze tija.

Mojawapo, alisema Waziri Mkenda, ongezeko la tija litawezekana kwa wakulima kupata mbolea na pembejeo zingine kwa bei rahisi na muda muafaka hatua itakayowafanya wakuze kipato chao na uchumi wa nchi kukua.

Ameitaka bodi hiyo kukutana na wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vya kuzalisha mbolea kujadili na kuweka mikakati ya kufanya

wakulima wapate mbolea bora na kwa bei rahisi.

Katika hatua nyingine Profesa Mkenda ameagiza mamlaka hiyo kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kutoa elimu ya upimaji afya ya udongo kwa wakulima ili watambue aina ya udongo na mbolea inayofaa kwa aina hiyo ya udongo ili waweze kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao.

Waziri huyo wa Kilimo alibainisha kuwa hali ya upatikanaji mbolea nchini umefikia tani 631,660 mwaka huu Februari kati ya mahitaji ya tani 718,051 na kuwa serikali itaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya mbolea hapa nchini ili kupunguza utegemezi wa mbolea toka nje ya nchi.

Kwa upande wake Veronica Soko mjumbe wa bodi ya TFRA anayewakilisha wakulima wadogo kupitia MVIWATA aliomba serikali kuweka utaratibu wa kuvikopesha vyama vya ushirika vya wakulima ili wanunue mbolea kwa mfumo wa pamoja hatua itakayosaidia wakulima kuipata kwa bei nafuu.

Mkulima huyo wa mpunga toka Madibira wilaya ya Mbarali alibainisha kuwa wanachama wake wamefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mpunga kwa njia ya umwagiliaji na matumizi ya mbegu na mbolea bora kuongeza uzalishaji toka gunia 20 hadi 25 kwa hekta hadi kufika tani 7 hadi 10 mwaka 2019.

“Vyama vya ushirika vikitumika kuagiza mbolea kwa mfumo wa pamoja itasaidia wakulima kufikishiwa bidhaa hiyo kwa bei nafuu huku ikiwa iezingatia aina ya zao wanalozalisha “ alisema Soko.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Profesa Anthony Mshandete ameipongeza serikali kwa maelekezo ambayo imekuwa ikiyatoa hatua ianayosaidia bodi yake kuwafikia wakulima wengi kwa kufikisha mbolea inayohitajika kupitia mfumo wa ununuzi wa pamoja( BPS).

Profesa Mshandete amesema bodi hiyo ilioanzishwa kwa Sheria ya Mbolea Namba 9 ya mwaka 2009 itaendelea kuhakikisha inadhibiti ubora wa mbolea ili wakulima wanufaike na kuwezesha Kilimo kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa .

“Mkakati wetu ni kuhamasisha watanzania wengi waanzishe viwanda vya mbolea hapa nchini hali itakayosaidia kupata mbolea bora na yenye gharama nafuu hivyo kuachana na utegemezi wa mbolea toka nje ya nchi” alihitimisha Prof. Mshandete.

Takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania zinaonesha katika mwaka 2020 Tanzania imetumia Dola za Kimarekani Milioni 229.8 kuingiza nchini mbolea tani 659,197 toka nje ya nchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz