Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yakabidhiwa mitungi 10,000 ya gesi, makundi lengwa kufikiwa

GESII WEBB Serikali yakabidhiwa mitungi 10,000 ya gesi, makundi lengwa kufikiwa

Mon, 11 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Tanzania imekabidhiwa mitungi 10,000 ya gesi na Kampuni ya Taifa Gas, ili kuendeleza juhudi za kuhamaisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango, aliyemuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, katika kongamano la wanawake la kuhimiza matumizi ya nishati safi jijini Dodoma juzi, Machi 8, 2024 alipokea mitungi hiyo iliyokabidhiwa na meneja mkuu wa Taifa Gas, Devis Deogratius.

Akizungumza katika kongamano hilo, Deogratius aliipongeza Serikali kwa juhudi za kuipambania Tanzania, ili iwe miongoni mwa nchi zinazotamba duniani katika kutumia nishati safi ya kupikia.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Wizara ya Nishati na kuhudhuriwa na mamia ya wanawake kutoka pembe zote za nchi, Deogratius amesema mikakati iliyowekwa na Taifa Gas nchini inalenga kuhakikisha gesi inapatikana katika kila mlango wa Mtanzania.

“Taifa Gas katika mikakati yake itaendelea kufanya kazi na wadau wote wakiwamo Serikali kupitia Wizara ya Nishati, wabunge, Serikali za mikoa, wilaya na ngazi nyingine ili kufanikisha agenda ya matumizi ya nishati safi nchini,” amesema.

Makamu wa Rais, Dk Mpango alipongeza hatua ya Taifa Gas ya kutoa mitungi 10,000 na kusema itasaidia kuhakikisha makundi yanayostahili kupata gesi yanafikiwa.

Hata hivyo, katika kulisisitiza hilo, Dk Mpango alimtaka Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kuangalia uwezekano wa kupitia viwango vya kodi kwa majiko yanayotumia nishati safi ya kupikia, ili kuleta unafuu wa bei kwa wananchi wa kipato cha chini.

“Ninamtaka Waziri wa Fedha atazame uwezekano wa kupitia viwango vya kodi kwa majiko yanayotumia nishati safi ya kupikia na hasa kuanzia kipindi hiki ambacho maandalizi ya bajeti ijayo yanafanyika,” amesema Dk Mpango.

Bei ya gesi hutegemeana na kampuni, mfano, mitungi ya gesi ya ujazo wa kilo 3.5 ni Sh29,000, ujazo wa kilo sita ni Sh42,000, ujazo wa kilo 15 Sh92,000 na ujazo wa kilo 38 ni Sh195,000.

Pia, Dk Mpango amesisitiza kuwa katazo la Serikali la matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku, ni fursa ya uwekezaji kwa sekta binafsi katika kuzisaidia taasisi hizo kuona namna ya kuondoa changamoto ya upatikanaji wa nishati safi.

“Vilevile, hii ni fursa kwa taasisi za fedha kuchangia katika upatikanaji wa nishati safi ya kupikia. Natoa wito kwa taasisi za fedha kutengeneza bidhaa maalumu zitakazowezesha taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku kupata mikopo yenye riba nafuu, ili kuwekeza kwenye mifumo ya nishati safi ya kupikia,” amesema.

Pia, ametaka kongamano liainishe namna fursa za ujasiriamali katika kutumia nishati safi ya kupikia zitafahamika na kuchangamkiwa kwa kuongeza ajira na kuwezesha watu kujikwamua kiuchumi.

“Hamasa itakayotolewa ijumuishe fursa za mifuko ya mazingira, ikiwemo biashara ya kaboni ili kuwajengea uwezo wananchi na kunufaika na biashara hiyo,” anasema.

Dk Mpango amesema suala la gharama za upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ambazo bado ni kikwazo kwa kaya nyingi zenye vipato vya chini, linahitaji uwekezaji mkubwa na ubunifu ili kulifanikisha.

“Wakati Serikali inakamilisha taratibu za kuanzisha mfuko wa nishati safi ya kupikia, ili kuweka ruzuku itakayowawezesha wananchi wa kipato cha chini kumudu bei ya gesi, nawaomba wadau mbalimbali kusaidia utekelezaji kupitia mikopo midogomidogo, vikoba au vikundi vya kina mama kupitia ule utaratibu wa kukusanya fedha, ili kuhakikisha mama anapata vyombo vya ndani,” amesema.

Amesema fursa mojawapo ambayo inaweza ikasaidia kupunguza changamoto ya gharama ni matumizi ya mapato yatokanayo na biashara ya hewa ukaa.

“Hivyo, vijiji na watu binafsi wanaopata mapato kutokana na biashara hiyo tunawahimiza wayatumie kugharamia nishati safi ya kupikia,” amesema.

Dk Mpango amezitaka taasisi za utafiti, sekta binafsi na wadau wengine kubuni teknolojia rahisi na zitakazopatikana kwa gharama nafuu, ili kuharakisha uhamaji kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu.

“Kwa mfano, kubuni na kueneza matumizi ya majiko yanayotumia nishati safi kuwezesha kupika chakula kinachoiva kwa muda mrefu kama maharage na kande badala ya kutumia mkaa au kuni.

“Natoa wito kwa sekta binafsi kuunga mkono na kuchangia katika kampeni ya kuondokana na matumizi ya nishati chafu,” amesema.

Hii ni mara ya pili kwa kampuni ya Taifa Gas kudhamini kongamano la nishati baada ya lile la mwaka 2022 lililofanyika jijini Dar eses Salaam.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema kongamano hilo ni utekelezaji wa ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoibeba kwa Afrika.

Amesema ahadi hiyo pia ni kwa Watanzania ya kumtua mama kuni kichwani kwa kumpatia nishati safi ya kupikia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live