Katika kukabiliana na uhaba wa chakula na uuzaji nje ya nchi, Serikali imeanza ununuzi wa mahindi na mpunga.
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), umeanza ununuzi huo kwa msimu wa 2023/24 unaofanyika katika kanda nane zinazojumuisha mikoa 17 nchini. Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na NFRA katika gazeti la Mwananchi toleo la jana, ununuzi wa akiba ya chakula ulianza Juni 22, mwaka huu.
Juni 15, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka Watanzania kutumia vizuri chakula, huku wakijihadhari na njaa inayoweza kuikumba dunia kutokana na sababu kadhaa, ikiwamo mabadiliko ya tabianchi, athari za Uviko-19 na vita kati ya Russia na Ukraine. Rais Samia alisema kutokana na tishio hilo la njaa na mfumuko wa bei duniani, Serikali inakamilisha mchakato wa kununua na kuhifadhi chakula cha kutosha katika maghala ya Taifa kwa tahadhari, lengo likiwa ni kuwahakikishia Watanzania uwepo wa chakula. Hayo yanafanyika kukiwa na malalamiko kutoka kwa wabunge waliochangia hoja katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2023/24 wakieleza kuporomoka kwa bei ya mahindi nchini. Kwa mujibu wa michango ya wabunge, bei ya mahindi imeporomoka kwa sababu ya zuio la Serikali juu ya usafirishaji wa mazao nje ya nchi. Hata hivyo, katika majibu yake kwa wabunge, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema Serikali haijazuia mahindi kusafirishwa nje, lakini msimamo utabaki vilevile kuwa, lazima wafuate sheria na walipe kodi halali. Alisema Serikali imetoa Sh320 bilioni kwa NFRA kwa ajili ya kununua mahindi kwa kati ya Sh600 hadi Sh800 kwa kilo. Wakala kupitia tangazo la jana, inanunua kilo moja ya mahindi kwa kati ya Sh600 na Sh1,000, huku mpunga ukinunuliwa kwa kati ya Sh900 na Sh1,000 kwa kilo moja. Hayo yakifanyika, ripoti ya Tathmini ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya kila mwezi iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika mwaka ulioishia Mei 2023, inaonyesha hifadhi ya chakula ilikuwa imeshuka kutoka tani 80,123 Machi hadi tani 63,808 Aprili mwaka 2023. Ripoti ya hali ya uchumi ya Mei mwaka huu inaeleza licha ya kushuka kwa hifadhi ya chakula, pia bei za mahindi zilishuka kutoka Sh119,484 kwa gunia la kilo 100 hadi kufikia Sh108,038 kati ya Aprili na Machi. Bei ya mchele iliongezeka hadi kufikia Sh300,067 kutoka Sh294,811 kwa ujazo uliokuwapo awali. NFRA katika tangazo hilo inasema kwa kuanzia itafungua vituo vya ununuzi wa mahindi kwenye kanda zenye uzalishaji na upatikanaji mkubwa wa nafaka. Kanda hizo ni Songea (Ruvuma), Makambako (Iringa na Njombe), Songwe (Mbeya, Songwe), Sumbawanga (Rukwa na Katavi), Dodoma (Singida na Dodoma), Arusha (Manyara na Arusha) na Shinyanga (Kigoma na Tabora). Mpunga utanunuliwa katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Songwe, Mbeya na Tabora. “Utaratibu wa ununuzi wa nafaka kupitia vyama vya ushirika/vikundi vya wakulima, wafanyabiashara na mawakala utafanyika kupitia makubaliano yatakayofikiwa baina ya makundi hayo na kanda za NFRA. Malipo yatafanyika ndani ya siku tatu baada ya taratibu zote kukamilika,” inaeleza sehemu ya tangazo hilo.
Kauli za wachumi Akizungumzia hatua ya NFRA kuanza ununuzi wa nafaka, Dk Donath Olomi, mtaalamu wa biashara na uchumi alisema kinachofanywa sasa ni hatua nzuri inayoweza kuinusuru nchi kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza chakula nje ya nchi endapo kutakuwa na upungufu. Hata hivyo, alitoa angalizo kuwa ni lazima bei inayotolewa imnufaishe mkulima ili apate hamasa ya kuendelea na kilimo. Tofauti na hilo, alisema mkulima atakazimika kubadilisha aina ya mazao anayolima ili kujiingizia kipato. “Ni muhimu sana kutunza chakula, tusipokuwa na chakula itabidi tuagize kutoka nje, tutatumia fedha nyingi za kigeni, lakini pia tunaponunua kutoka kwa wakulima tununue kwa bei itakayomnufaisha,” alisema. Mchumi Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora alisema wakati Serikali ikianza ununuzi ni vyema ikafanya utafiti kwa nini bei imeshuka. Alishauri kuwapo bei elekezi na shindani ili kumnufaisha mkulima. “Tujue sababu ni nini za kushuka kwa bei huku sokoni, baada ya hapo wakulima waambiwe kuwa hiki ndicho kimesababisha ili kuondoa sintofahamu iliyopo,” alisema Profesa Kamuzora.