Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yajitosa sakata la malori yaliyokwama DRC

MALORI 1 780x470 itaifa Serikali yajitosa sakata la malori yaliyokwama DRC

Sun, 22 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar es Salaam. Serikali imeanza juhudi za kukwamua malori 250 yaliyokwama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kufuatia madai ya baadhi ya kampuni za madini kudaiwa kodi nchini humo.

Hatua hiyo inakuja wakati Chama cha Madereva Tanzania (TADWU) kikiziomba Serikali ya Tanzania na ile ya DRC kukutana na kutafuta suluhu.

Mbali na malori hayo 250, madereva na wasaidizi wao zaidi ya 500 wamekwama nchini humo kwa siku 45 sasa, kwa kile kinachoelezwa kuwa baadhi ya migodi ya madini nchini humo inadaiwa kodi na Serikali ya DRC.

Akizungumza na Mwananchi jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba alisema Serikali inatambua suala hilo na tayari imeshaanza kutafuta suluhisho kupitia ubalozi wake.

“Madereva wameathiriwa na operesheni ya kukusanya kodi ya Serikali ya DRC. Kwa hiyo tumeshaanza juhudi kupitia balozi wetu na kesho atakwenda kukutana na Waziri wa Madini wa nchi hiyo,” alisema.

Hata hivyo, jana Balozi wa Tanzania nchini DRC, Said Mshana hakupatikana kuzungumzia suala hilo, baada ya simu yake kuita kwa muda mrefu.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa TADWU, Schubert Mbakizao, alisema suala hilo limeonekana kuchukua muda mrefu kutatuliwa kwa kuwa wamiliki wa malori wamejigawa, ambapo mpaka sasa vipo vyama vitatu na kila mmoja anatafuta watu wa kukutana nao kutatua tatizo hilo.

“Mpaka sasa katika hawa wamiliki kuna wanaojiita TAT, Chama cha Wamili wa Malori Tanzania (Tatoa) na Chama cha Wamiliki malori wa kati na wadogo Tanzania (Tamstoa), kila mmoja anajua anapita njia yake kuangalia namna gani ya kunasua magari yao, jambo hilo linafanya mamlaka kutolichukulia kwa ukubwa suala hilo,” alisema.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tamstoa, Chuki Shabani, alisema haoni kama kujigawa huko kuna athari kwa kuwa wote wanapambania kitu kimoja na anatamani kungekuwa na vyama vingi zaidi.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), Omar Kiponza alisema kuwa vyama vyote vinavyoundwa vinakuwa na malengo yake, hivyo haoni kama kuna shida na ndiyo maana Serikali inavisajili.

“Huyo anayeongea kwamba tumegawanyika atakuwa haelewi maana ya kuwepo kwa vyama hivi vya hiari, kwani kama tungekuwa tuna matatizo basi hata serikali isingekubali kutusajili,” alisema Kiponza.

Kuhusu kukamatwa kwa magari yao, Kiponza kinachofanywa na Congo ni uhuni kwani wanatumia magari yao kama shinikizo la kampuni hizo za madiini kuwalipa kodi jambo ambalo sio sawa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live