Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yajitosa mgogoro wa kahawa Hai

45867 PIC+KAHAWA Serikali yajitosa mgogoro wa kahawa Hai

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kampuni ya Tudeley Estates Limited ya Uingereza imetakiwa kurudi Tanzania kufanikisha utatuzi wa mgogoro wa uwekezaji katika kilimo cha kahawa wilayani Hai, Kilimanjaro.

Kampuni hiyo ndiyo iliingia mkataba na vyama vya ushirika vinavyojishughulisha na uwekezaji katika Kilimo cha kahawa wilayani humo (Murososangi), lakini ghafla akaibuka mwekezaji mpya ambaye mkataba wake haujulikani.

Mgogoro huo umewalazimu mawaziri wawili, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na yule wa Uwekezaji katika Ofisi ya waziri mkuu, Angela Kairuki kufanya mkutano na wawekezaji, vyama vya ushirika na wadau wengine kujaribu kutafura suluhisho.

Dk Mpango alisema Murososangi iliingia mkataba na Tudeley Estates Limited inayomiliki mashamba yenye ukubwa wa ekari 2,054 katika eneo la Kibo na Kikafu ili kuendeleza zao la kahawa kuanzia mwaka 1998.

Alisema baada ya mwekezaji huyo, Conrad Legg kuonesha nia ya kutoendelea na uwekezaji huo aliondoka nchini, wakaja wawekezaji wengine kutoka Ujerumani ambao waliingia mkataba na Kampuni ya Tudeley Estates Limited, kwa kununua hisa bila kuvishirikisha vyama vya ushirika vilivyoingia mkataba wa awali.

“Aliyeingia mkataba na Murososange arudi nchini ili kutatua mgogoro huu ili kuona wananchi wanawezaje kuingia mkataba mwingine na mwekezaji mpya ambao utalinda maslahi ya wananchi,” alisema Dk Mpango.

Alisema wanaushirika hao wanataka mwekezaji wa kwanza arudi nchini ili wavunje mkataba wa awali kwa kuwa haujaisha muda wake, hivyo hawawezi kuingia mkataba na mwekezaji mpya wakati ule wa awali unaendelea.

Kwa mujibu wa waziri huyo, mwekezaji mpya kutoka Ujerumani, Marcus Shiber alianza kuleta fedha katika eneo la uwekezaji na kulipa baadhi ya kodi za mtangulizi wake, madeni, mishahara na kuboresha miundombinu ya mashamba hayo bila muafaka na Murososange.



Chanzo: mwananchi.co.tz