Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yajitosa kuwezesha benki nchini

383c071a48b216532baee7321fff15ed Rais Samia akizindua jengo la Makao makuu ya CRDB jijini DSM

Sat, 5 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imetenga Sh. Trilioni moja ikiwa ni mpango mahususi wa kuziongezea nguvu benki, ili ziweze kukopeshwa kwa riba ndogo isiyozidi asilimia 10.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la makao makuu ya benki ya CRDB jijini Dar es Salaam leo, Rais Samia Suluhu amesema serikali imeanzisha mpango huo kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Serikali kupitia Benki Kuu imeanzisha mpango mahususi wa kuwezesha sekta za kibenki kupata mikopo yenye riba nafuu, ambapo Benki Kuu imetenga jumla ya Sh. Trilioni moja kwa ajili ya kuwakopesha mabenki kwa masharti nafuu sana,” amesema Rais Samia na kuipongeza benki ya CRDB kwa kuitikia wito wa Serikali kupunguza riba.

Ametoa wito kwa benki kuhakikisha fedha watakazokopeshwa na Serikali kwa riba ndogo zisitumike kulipa madeni yao, bali zielekezwe kukopesha sekta binafsi kama ilivyokusudiwa.

Pia Rais ametaka benki kutanua wigo na kutoka nje ya nchi kwenda kufungua matawi, ili kuimarisha uchumi na kuleta faida nchini.

“Mwanangu Juma Nature kuna wimbo wake mmoja anasema kwani wao wameweza wana nini, hata sisi tushindwe tuna nini, wao wana akili na sisi tuna akili, kwa hiyo tutaweza, popote mnapoweza kwenda nendeni kwa nguvu, mabenki ya nje yanakuja Tanzania kwa nini sisi tushindwe?

“Katika kutoa fursa na kuongeza ajira kwa sekta binafsi, bodaboda, mama ntilie naomba mabenki muyashike hayo makundi, muende nayo vizuri,” amesema Rais na kuongeza kuwa:

“Nimepata taarifa benki mna utaratibu wa kurudisha kwa jamii, naambiwa mwaka jana kupitia Corporate social responsibility (CSR), CRDB mmetumia Sh. Bilioni 1.8 katika kutoa huduma za kijamii mwaka jana 2021 ikiwemo afya, elimu uwezeshaji wa vijana, mazingira na na kadhalika, nami ni shahidi katika hili, nawapongeza sana.”

Pia aliwapongeza taasisi za fedha kwa kurasimisha sekta isiyo rasmi, lakini akiwasihi pia wasaidie Wamachinga waweze kusimama vizuri na waweze kukopeshana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live