Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amesema serikali imejipanga kuwasaidia wanawake katika biashara ikiwemo kuwapa mitaji na teknolojia sahihi ya ufanyaji biashara na kuweka miundombinu wezeshi ili waweze kuingia kwenye soko huru la biashara barani Afrika.
Hayo ameyasema leo Desemba 7,2023 jijini Dar es salaam kwenye kongamano la wanawake kwenye biashara chini ya mkataba wa eneo huru la biashara barani Afrika( AfCFTA) linaloendelea kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius nyerere JNICC.
Amesema nchi imeendelea kuimarisha upatikanaji wa mitaji kupitia taasisi zafedha ikiwemo mabenki na taasisi nyingine lakini pi wizara kupitia SIDO wanatoa mafuzo ya ujasiliamali lakini pia mitaji(mikopo) lengo likiwa kumuwezesha mwanamke katika biashara.
“Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara kwa wanawake tu lakini wizara kupitia Shirika letu la viwanda vidogo SIDO tunatoa mafunzo ya ujasiliamali na pia mitaji kwa mkopo lakini pia kuna fedha zinazokopeshwa kupitia halmashauri kwa ajili ya kuwasaidia wanawake vijana na watu wa makundi maalum”amesema Kigahe.
Ameongeza kuwa fedha zinazotolewa na halmashauri zimeboreshwa ili kusaidia wajasiliamali kukuza biashara zao na kuwa kubwa ili ziweze kuingia kwenye ushindani kwenye masoko makubwa.
Amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo SIDO wanasaidia wajasiliamali hao kupata teknolojia rahisi na sahihi ili kuzalisha kwa wingi bidhaa zao kwenye maeneo yao.
“Eneo la biashara Afrika lina nchi zaidi ya 55 ambazo zinaweza zikafanyabiashara ya pamoja hivyo Tanzania wanafursa hiyo kubwa ya kufanyabiashara kwani kuna bidhaa nyingi zinazozalishwa ikiwemo mkonge”amesema Kigahe.
Akizungumzia mkonge amesema ni moja ya bidhaa ambayo inahitajika sana kwenye soko la kimataifa hasa Bara la Afrika kwani mkonhe ukichakatwa inatumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo urembo na ujenzi.
“Mkonge unatumika katika ujenzi na unasaidia kupunguza joto hii teknolojia ambayo tukiitumia hata sisi itasaidi kupunguza uharibifu wa mazingira lakini pia gharama za uendeshaji ikiwemo kufunga viyoyozi”
Amesema serikali imeboresha miundombinu ya usafirishaji wa bidhaa hivyo ametoa wito kwa wajasiliamali kushiriki ili kuchangamikia fursa lakini wanawaweke wajasiriamali kushirikiana na wengine kutoka nchi nyingine ili kubadilishana uzoefu na kutengeneza mtandao.
Kwa upande wake katibu mkuu mstaafu UWT bi Asma Mwilima amesema wanawake wafanyabiashara wanapata vikwazo mbalimbali pindi wanaposafirisha bidhaa zao nje ya nchi ikiwemo TRA hivyo kongamano hilo ni la muhimu kwani wanatumia jukwaa hilo kujadili changamoto zao na kuzifikisha kwa wahusika.
Nae,waziri wa maendeleo ya jamii,jinsia wazee na watoto Zanzibar Riziki Pembe Juma ametoa rai kwa wanawake kujitokeza kwenye makongamano hayo kwani yanatoa fursa mbalimbali kwa wanawake hasa katika kujiendeleza kibiashara.
“Niwaombe sana wanawake wenzangu wa Bara na Zanzibar tutumie fursa ambayo Marais wetu wametusogezea ili kuona wanawake tunafarijika na kuondokana na utegemezi wa kiuchumi na ukizingatia mwanamke sasa ameshakuwa Rais hivyo hatupaswi kurudi nyuma tunapaswa kwenda mbele”amesema.