Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yajipanga kuongeza pensheni kwa wastaafu

Pic Fedha Data Wastaafu Joyce Ndalichako, Waziri wa Kazi, Vijana , Ajira na Wenye Ulemavu

Tue, 20 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imejipanga kuangalia uwezekano wa kuongeza pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu mara baada ya tathimini ya uhimilivu na uendelevu katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii itakayofanyika mwaka 2022/2023

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ulyakulu, Rehema Migila.

Katika swali lake la nyongeza, Rehema amesema waliostaafu kuanzia mwaka 2010 kurudi nyuma, pensheni yao ni ndogo sana na haikui.

“Serikali haioni sababu ya kuongeza pensheni yao ambayo haikui,”amehoji Rehema.

Akijibu swali hilo, Profesa Ndalichako amesema mifuko hufanya tathimini kuangalia uhimilivu na uendelevu na ndio inavyoweza kuangalia kama inaweza kuongeza mafao.

“Serikali imepanga kufanya tathimini ya mifuko ya hifadhi ya jamii mwaka 2022/2023, na baada ya tathimini hiyo ndio tutaona uwezekano wa kuongeza kulingana na uwezo wa mifuko yetu,”amesema.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo aliuliza kuna mpango gani wa kuwapatia warithi wa mstaafu asilimia 67 ya michango yake pindi anapofariki.

Akijibu swali hilo, Profesa Ndalichako amesema Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), hulipa mafao ya mkupuo (lump sum) ambayo ni jumla pensheni ya miezi 36 (sawa na miaka 3) kwa wategemezi.

Amesema kwa upande wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), mstaafu anapofariki Mfuko hulipa mafao ya mkupuo sawa na pensheni ya miezi 24 kwa wategemezi.

Amesema ulipaji wa mafao huzingatia Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2018 na marekebisho yake ya mwaka 2019 na Kanuni za Mafao za mwaka 2018 kama zilivyorejewa mwaka 2022.

Profesa Ndalichako amesema mafao yanayolipwa hayazingatii asimilia ya michango isipokuwa wastaafu na wategemezi hulipwa mafao kulingana na kanuni zinazoongoza ulipaji wa mafao ya pensheni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live