SERIKALI imelieleza Bunge kuwa diplomasia ya uchumi ni dhana kuu katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje yenye dhamira ya kuwa na ushirikiano na uhusiano wa kimataifa wenye manufaa ya kiuchumi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax alisema hayo bungeni Dodoma jana wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Dk Tax aliwaeleza wabunge kuwa dhana ya diplomasia ya uchumi inazingatiwa katika malengo yote ya sera ya mambo ya nje na hata malengo yanayoonekana ya kisiasa yanachukuliwa kuwa ni sehemu ya kutoa fursa ya kuwa na uhusiano wenye manufaa ya kiuchumi.
Alisema utekelezaji wa diplomasia ya uchumi utaendelea kuwa kipaumbele cha serikali ili kunufaika na fursa za kiuchumi na kijamii ikiwemo masoko ya nje kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini, kuvutia uwekezaji, kukuza utalii na kuendeleza miradi.
Dk Tax alisema utekelezaji wa diplomasia ya uchumi unahusisha sekta za kiuchumi na jamii zilizopo katika sekta ya umma na sekta binafsi.
Dk Tax alitaja mambo yanayozingatiwa katika diplomasia ya uchumi ni kutafuta masoko ya bidhaa zetu, kutafuta fursa za kiuchumi katika sekta mbalimbali, mikopo na misaada yenye masharti nafuu.
Alitaja mengine ni kuvutia uwekezaji na mitaji, kuvutia watalii, kubidhaisha lugha ya Kiswahili, fursa za elimu, utaalamu na ujuzi na ajira nje ya nchi.
“Kwa kutambua kuwa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ni suala mtambuka na ili kuongeza tija katika utekelezaji wake, wizara inaendelea na maandalizi ya mpango na mkakati wa kitaifa wa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi,” alisema Dk Tax.
Alisema mpango huo utawezesha wadau kutoka sekta zote husika, sekta ya umma na sekta binafsi kushiriki kikamilifu na kwa tija zaidi.
Dk Tax alisema wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau ndani na nje ya serikali imekamilisha maandalizi ya marekebisho ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2023 na mkakati wa utekelezaji.
Alisema marekebisho ya sera hiyo yameendelea kuweka msisitizo katika diplomasia ya uchumi.
“Aidha, maeneo mapya yaliyojumuishwa ni pamoja na masuala ya diaspora; uchumi wa 26 buluu; mazingira na mabadiliko ya tabianchi; na kukuza na kubidhaisha lugha ya Kiswahili,” alisema Dk Tax.