Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaja na mipango kusimamia mabonde ya maji

Thu, 15 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imeandaa mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa maji kwenye mabonde tisa yaliyopo nchini ili kupambana na changamoto zinazohatarisha kutoweka kwa rasilimali hiyo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Emmanuel Kalobelo amesema mipango hiyo inatoa muongozo wa namna maji yanavyoweza kutumika kwenye bonde husika na aina ya miradi inayopaswa kujengwa.

Akizungumza kwenye mkutano wa pili wa Jukwaa la Sekta Mtambuka katika usimamizi wa raslimali za maji leo Novemba 14, 2018, Kalobelo amesema mipango hiyo inashirikisha sekta zote muhimu zinazotumia maji.

“Tuliona kwamba haiwezekani sekta ya maji ikawa ndiyo pekee inayosimamia matumizi sahihi wakati watumiaji ni sekta zote ndio maana tumekuja na mipango hii,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa Raslimali za Maji, Dk George Lugomela alisema mipango hiyo itasaidia kumaliza migogoro ya maji kwa sababu inaelekeza mgawanyo sahihi na namna ya kuongeza pale inapoonekana rasilimali hiyo haitoshelezi mahitaji.

 “Maji yanatumika kwenye uzalishaji umeme, kilimo, viwanda, majumbani, mazingira, utalii na sekta nyingine nyingi kwa hiyo kila mdau anapaswa kupata na kusoma ili ajue aliko ni shughuli gani imeainishwa,” amesema.

Mabonde yaliyopo nchini ni Rufiji, Pangani, Ziwa Tanganyika, Wami Ruvu, Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa, Rukwa na Bonde la Kati.



Chanzo: mwananchi.co.tz