Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaitaka TRA kutofungia maduka ya wasiolipa kodi

34152 Pic+tra Waziri Philip Mpango

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepigwa marufuku kufunga maduka na biashara za watu kwa kisingizio cha kutolipa kodi, badala yake imetakiwa kukaa meza moja na wafanyabiashara ili kujadiliana nao.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitoa agizo hilo jana wakati akitoa taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa na utekelezaji wa bajeti ya Serikali katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2018/19.

“Utaratibu wa kumfungia biashara mfanyabiashara anayedaiwa kodi ili kumshinikiza alipe sasa usitishwe mara moja, isipokuwa kwa wakwepa kodi sugu na hapo lazima kuwe na kibali cha kamishna wa mkuu wa TRA, nataka mjikite katika kutoa elimu siyo vitisho,” alisema Dk Mpango.

Waziri huyo alikemea matumizi mabaya ya lugha, vitisho na ubabe dhidi ya walipakodi wenye historia nzuri akitaka yasipewe nafasi na itakapothibitika mtumishi wa TRA amekwenda kinyume awajibishwe kwa kuzingatia tararibu za kiutumishi.

Dk Mpango alisema hata Rais John Magufuli amekwishaagiza utaratibu wa kufungia maduka usitishwe alipofungua kikao kazi cha TRA Desemba 10, hivyo amri hiyo inapaswa kutekelezwa.

Kiongozi huyo aliagiza TRA kujikita katika kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili waone faida na thamani ya kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi yao na akawataka kupambana na wakwepa kodi hasa katika maeneo ya bandari bubu ambako alisema dawa yao ni kuwalipisha kodi na kutaifisha bidhaa zilizokwepa kulipiwa.

Hali ya maisha

Dk Mpango alisema hali ya maisha ya Watanzania imeendelea kuimarika hasa waliopata ajira na katika shughuli za uchumi zinazokua kwa haraka kama ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, upanuzi wa bandari na viwanja vya ndege ambao wengi wamejenga nyumba bora.

Alisema ukuaji mzuri wa uchumi uliisaidia Serikali kuongeza ukusanyaji wa mapato na kugharamia uboreshaji wa huduma za jamii katika zahanati, elimu, dawa, maji na kuimarisha uzalishaji wa umeme na kuusambaza vijijini.

Maduka ya fedha

Dk Mpango alisema mabadiliko yaliyofanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Juni 2017 yaliweka masharti ya uendeshaji wa maduka ya kubadilishia fedha ambapo yamesababisha zaidi ya nusu ya maduka hayo kufutwa kwa kutokidhi vigezo.

“Tuliweka masharti kuwa kiwango cha chini cha mtaji wa maduka yaliyoko daraja A kiongezeke kutoka Sh100 milioni hadi 300 milioni na daraja B kutoka Sh250 milioni hadi 1 bilioni, hivyo zoezi la usajili limeendeshwa na tulikuwa na maduka 297, lakini tumetoa leseni kwa maduka 109 ndiyo yamekidhi vigezo,” alisema

Mwenendo wa benki

Waziri Mpango alisema sekta ya benki imeendelea kuimarika na kutengemaa ikiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha zaidi ya kiwango kunachotakiwa kisheria ambapo mitaji ya benki ukilinganishwa na rasilimali zao ni asilimia 16.3 wakati kiwango kinachotakiwa ni asilimia 10.

Waziri alisema katika kipindi cha Januari hadi Novemba, sekta hiyo ilipata faida ya Sh285.4 bilioni ikilinganishwa na Sh317 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka jana wakati mikopo chechefu iliendelea kushuka hadi kufikia asilimia 9.7 ya mikopo yote mwezi Septemba 2018 kutoka asilimia 12.8 iliyorekodiwa Desemba 2017.

Thamani ya shilingi

Waziri Mpango alisema shilingi ya Tanzania imeendelea kuwa tulivu katika kipindi cha Julai hadi Novemba ambapo Dola ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa Sh2,276 ikilinganishwa na Sh2,235 katika kipindi kama hicho 2017.

Alisema ukwasi kwenye benki za biashara uliongezeka na riba katika masoko ya fedha zilipungua.

Alisema riba ya siku moja katika soko la fedha baina ya benki ilishuka kutoka asilimia 3.72 mwezi Oktoba 2017 hadi wastani wa asilimia 2.29 Oktoba, mwaka huu. Kwa upande wa riba ya dhamana ya Serikali zilipungua kutoka asilimia 9.41 na kuwa asilimia 7.40 kwa mwezi Oktoba huku riba ya mikopo iliyotolewa na benki ikipungua kutoka wastani wa asilimia 18.1 kati ya Julai 2017 na kufikia asilimia 17.3 Oktoba 2018.

Akiba ya fedha za kigeni

Hadi mwishoni wa Novemba 2018, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola za Marekani 5,079.0 milioni kiasi alichosema kinatosha kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi cha miezi mitano.

Misaada na mikopo

Dk Mpango alisema washirika wa maendeleo waliahidi kuchangia bajeti ya Serikali kwa Sh2.67 trilioni, lakini hadi Novemba walikuwa wamechangia Sh498.5 bilioni ambazo ni asilimia 54 ya kiwango walichopaswa kuwa wamechangia katika kipindi hicho cha Sh928.7 bilioni.

Alizitaja sababu za kuchelewa kutolewa kwa fedha na wahisani kuwa ni masharti magumu wanayotoa na majadiliano kuchukua muda mrefu.

Dk Mpango alisema hadi Septemba jumla ya deni la Serikali lilifikia Sh49.37 trilioni kutoka Sh47.82 trilioni kwa kipindi kama hicho 2017, ambapo lile la ndani ni Sh13.64 trilioni na la nje ni Sh35.72 trilioni, lakini alisisitiza kuwa bado ni himilivu.



Chanzo: mwananchi.co.tz