Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaipa TBA maagizo mradi wa nyumba za watumishi

Tba Pic Serikali yaipa TBA maagizo mradi wa nyumba za watumishi

Thu, 24 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya ameagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Mwanza kukamilisha kwa wakati na kujenga kwa ubora unaotakiwa jengo la makazi ya watumishi wa umma linalojengwa katika mtaa wa Ghana Wilaya ya Ilemela mkoani humo, ifikapo Julai 20, 2024.

Ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa sita litakalobeba familia 14 ulianza Januari 20, 2023 kwa gharama ya Sh7.7 bilioni na kutarajiwa kukamilika na kukabidhiwa Julai 20, 2024 ukihusisha pia majengo mawili ya ghorofa moja yenye vyumba 30 kwa ajili ya shughuli za kibiashara yatakayosaidia kutoa huduma kwa wakazi watakaokuwa wakiishi kwenye jengo hilo.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 23, 2023 wilayani Ilemela baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, Kasekenya ameitaka TBA kuhakikisha ubora wa majengo hayo unafikiwa kama ulivyosanifiwa na muda wa ujenzi wa miezi 18 uliopangwa unatimizwa kwa wakati ili kukata kiu ya mahitaji ya nyumba za makazi ya watumishi wa umma.

“Naona mmefikia asilimia 25 ya ujenzi na sehemu kubwa hapa mnajenga, kusimamia na baadhi ya vifaa yakiwamo matofali mnatengeneza wenyewe hivyo hatutegemei kutumia vifaa ambavyo siyo bora na mradi kuwa chini ya kiwango, kwahiyo tunategemea jengo hili liwe moja kati ya majengo bora ya kisasa ili lengo la kusaidia watumishi kuishi mahali pazuri lifanikiwe,

“Niwaombe viongozi wa mkoa na wilaya kuhakikisha wanatembelea hapa na kuwasimamia hawa ili kunapotokea changamoto itatuliwe mara moja na tusipungukiwe na kitu. Nimeridhika na kazi inayoendelea naamini utakapokamilika tutakuwa tumepata majengo mazuri ya kisasa kwa ajili ya watumishi,” amesema Kasekenya

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo uliopo eneo la Ghana Estate lenye ukubwa wa mita za mraba 13,300, Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Mwanza, Moses Urio amesema awamu ya kwanza itakuwa na sakafu saba zitakazobeba familia 14 na kila sakafu itakuwa na apatimenti mbili zitakazokuwa na vyumba vitano, huku ukiambatana na ujenzi wa majengo mawili ya ghorofa moja ya kibiashara yatakayouwa na vyumba 30 na kutoa huduma kwa wakazi watakaokuwa wakiishi kwenye jengo hilo.

Amesema mradi huo unaotekelezwa kwa fedha za ndani za TBA una manufaa mbalimbali kwa wakazi wa jiji la Mwanza na Tanzania kwa ujumla ikiwamo kupunguza changamoto ya uhaba wa makazi kwa watumishi wa umma hivyo kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika kutoa huduma kwa jamii na kuboresha kipato cha wananchi kupitia biashara zitakazofanyika katika majengo ya kibiashara.

“Ubora wa kazi unazingatiwa na kusimamiwa kwa karibu kupitia wataalam wetu wanaotemebelea mradi na kufanya ukaguzi pamoja na vikao mbalimbali, vifaa vya ujenzi vinavyotumika katika mradi huu vinafanyiwa vipimo vya maabara kuhakiki ubora wake kabla ya kuanza kutumika na utekelezaji wa mradi huu umezingatia upatikanaji wa vibali mbalimbali vya ujenzi kwa mujibu wa sheria na taratibu katika bodi na taasisi mbalimbali ambazo zinahusika,”amesema Urio

Chanzo: www.tanzaniaweb.live