Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yahamasisha ujenzi viwanda vya nafaka

88c18bb2be1ce5dc512f09e358460a46.jpeg Serikali yahamasisha ujenzi viwanda vya nafaka

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imesema itaendelea kuhamasisha wawekezaji kujenga viwanda vya nafaka ili kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na kumaliza changamoto ya usafirishaji wa mazao kwenda nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha kuchakata nafaka na matunda cha Segera kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga.

Kigahe alisema ongezeko la viwanda vya kuchakata nafaka vitasaidia wakulima kupata soko la uhakika la mazao yao na kuachana na kuuza mazao maeneo mengine.

“Sasa mwarobaini wa nafaka zetu kukosa ubora utakwisha kwani kupitia uwepo wa viwanda hivi utasaidia kumaliza changamoto ya usafirishaji wa nafaka nje ya nchi,” alisema Naibu Waziri.

Aidha, alisema uwepo wa kiwanda hicho itasaidia kuongeza thamani ya mazao na hivyo kuuza nje ya nchi bidhaa ambayo tayari imeshachakatwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela alisema mazingira mazuri yaliwekwa na serikali kwa kushirikiana na mkoa yamesaidia kuvuta wawekezaji wengi kuja kuwekeza kwenye sekta ya viwanda mkoani humo.

“Tayari tunatarajia viwanda vinne vya kuchakata nafaka kujengwa ndani ya mkoa wetu ndani ya mwaka huu pekee, hivyo ni imani yangu wakulima wataweza kupata soko la uhakika la mazao yao,” alisema Shigela.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, John Kessy alisema mpaka kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda hicho utagharimu Sh bilioni 21.3 na kutoa ajira zaidi ya 600.

Alisema kiwanda hicho kitajengwa katika awamu tatu ambazo zitahusisha na kiwanda cha kuchakata nafaka, matunda na chakula cha mifugo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz