WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Tehama), Dk Faustine Ndugulile amezindua duka mtandao litakalowezesha wafanyabiashara, wajasiriamali na wenye viwanda kuweka bidhaa ili kupata soko kote duniani.
Dk Ndugulile alisema duka hilo limefunguliwa ili kutekeleza azma ya serikali ya kupeleka huduma kwa wananchi badala ya wananchi kufuata huduma.
Alisema jana katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), kuwa kupitia duka hilo mfanyabiashara yeyote ataweza kujiunga na kuuza au kununua bidhaa.
Duka hilo linaendeshwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade) na Shirika la Posta Tanzania.
"Huko mbele matumizi ya tehama yatakuwa makubwa sana, serikali inakwenda kwa watu si watu kwa serikali. Kupitia duka mtandao hili tunafungua milango ya mauzo na biashara ya Mtanzania yeyote aonekane dunia nzima bila kupitia dalali," alisema Dk Ndugulile.
Alisema wizara hiyo imeboresha huduma za posta kuwa za kidijitali zaidi kwa kuwezesha huduma kuwa kiganjani.
Dk Ndngulile alisema katika maboresho ya posta, wanaondoka kabisa katika mfumo wa anwani za kawaida za masanduku ya posta kwani umepitwa na wakati na sasa namba ya simu ni sanduku la posta la mtu.
Alisema wizara inaandaa sheria ya kusimamia utunzaji na ukusanyaji wa taarifa binafsi kuwaondoa watu katika anwani za SLP (Sanduku la Posta) na kuwa kimtandao.
Aliipongeza TanTrade kupitia Mkurugenzi wake Mkuu, Edwin Rutagerura kwa kazi wanayoifanya kubuni mambo mapya yanayoongeza huduma kwa Watanzania.
Waziri wa Biashara na Viwanda, Profesa Kitila Mkumbo alisema uzinduzi huo ni kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la taasisi za serikali zikiwemo wizara zifanye kazi kwa ushirikiano.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Tehama, Dk Zainabu Chaula alisema kuna maduka yamesajiliwa katika duka hilo mtandao hivyo watu wachangamkie fursa hiyo.
Kaimu Posta Masta Mkuu, Macrice Mbodo na Mkurugenzi Mkuu TanTrade, Rutagerura, walisaini makubaliano kushirikiana kuendesha duka mtandao.