Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yafunga mgodi wa Buziba

Serikali yafunga mgodi wa Buziba

Tue, 29 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Kutokana na ajali ya kutitia kwa mgodi wa dhahabu wa Buziba uliopo kata ya Lwamgasa wilayani Geita na kusababisha wachimbaji  wawili wadogo kupoteza maisha, Serikali imefunga mgodi huo hadi pale taratibu za kiusalama zitakapozingatiwa.

Wachimbaji hao, Jovin Baraka mkazi wa kata ya Nzera wilayani Geita na Jumanne Mgaya mkazi wa Jijini Dar es Salam walifukiwa na kifusi baada ya shimo la uchimbaji dhahabu waliloingia kinyemela usiku wa Oktoba 26, 2019 kutitia.

Akizungumza na  Mwananchi leo Jumatatu, Oktoba 28, 2019, Kamishna msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokozi mkoani Geita, Zablon Mhumha amesema mwili wa Jovin ulipatikana  jana Oktoba 27 majira ya saa 11 jioni huku mwili wa Jumanne ukitolewa leo Saa saba mchana.

Mhumha amesema mwili wa Jovin tayari umechukuliwa na ndugu zake kwa ajili ya maziko  na kwamba, mwili wa Jumanne umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Geita wakati  taratibu za kuwasiliana na ndugu zake wa Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maziko zikiendelea.

Amesema tayari ameagiza mashimo yote yaliyopo kwenye mgodi huo ambayo sio rasmi kufukiwa na kumtaka mmiliki wa eneo hilo kusitisha shughuli za uchimbaji hadi pale  taratibu za kiusalama zitakapokuwa zimechukuliwa na wao kujiridhisha kama hali ni salama.

Ofisa Madini wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda amesema mgodi waliofukiwa wachimbaji hao, mmiliki wake alikuwa ameomba kusitisha shughuli za uchimbaji kutokana na eneo kutokuwa salama lakini wachimbaji hao waliingia kinyemela .

Pia Soma

Advertisement

Amesema ofisi ya madini Geita imeanza ukaguzi wa migodi tangu Oktoba 2, 2019 kwa lengo la kukagua usalama na tayari wilayani Mbogwe migodi yote imekaguliwa.

Mapunda amesema kutokana na eneo la Lwamgasa kutokea ajali mara mbili kwa mwezi huu, timu ya ukaguzi kwa kushirikiana na jeshi la zimamoto inaanza ukaguzi maalumu kuanzia kesho ili kukagua mashimo yote ya wachimbaji wadogo.

“Ukaguzi wa migodi ni shughuli zetu za kila siku tumefanya Mbogwe na sasa tulikuwa twende Bukombe na Geita lakini kutokana na hii hali ya hewa tumeona tuanze ukaguzi kwenye maeneo ambayo ni ya uchimbaji wa wachimbaji wadogo na hii tutafanya na watu wa zimamoto,” alisema Mapunda.

Amesema lengo la ukaguzi huo ni kubaini pia maeneo yenye hatari ili wasitishe shughuli za uchimbaji lakini akawataka wenye migodi kuwa makini na kuzingatia  kanuni za usalama kabla ya kuingia ndani ya mgodi hususan kipindi hiki cha mvua.

Chanzo: mwananchi.co.tz