Serikali inafanya tathimini ya kina katika halmashauri nane nchini, kuangalia mahitaji na upungufu wa chakula ili kuzipeleka nafaka iwapo kutabainika kuna uhitaji.
Hatua hiyo inafanywa huku wakiwa tayari wamepeleka tani 3,000 za nafaka katika halmashauri tisa zilizothibitika kuwa na kasi kubwa ya upandaji wa bei za nafaka.
Hayo yamesemwa jana Jumamosi Oktoba 22,2022 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Milton Lupa wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya wakala huo katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita.
Amesema NFRA wamejipanga kuhudumia maeneo yatayodhibitika kuwa na mahitaji ya chakula au upungufu wa chakula baada ya kupata tathimini ya kina kuhusu maeneo halisi ambayo yameathirika.
“Kuna timu ambayo inafanya tathimini ya kina, tathimini ya awali ilishafanyika sasa hivi inafanyika tathimini ya kina itakapotoka sisi tunajipanga, tunatatua hilo tatizo la upungufu wa chakula,”amesema.
Lupa amezitaja halmashauri ambazo zimepelekewa tani 3000 za nafaka kuwa ni Bunda (Mara), Sengerema (Mwanza), Nzega (Tabora), Liwale na Nachingwea (Lindi), Longido (Manyara), Loliondo na Monduli (Arusha).
“Kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, wakala umefanikiwa kukabiliana na makali ya mfumko wa bei za nafaka katika maeneo yaliyohudumiwa, lengo la kupunguza makali, kwa kuongeza upatikanaji wa nafaka katika masoko na hivyo kuleta unafuu katika maisha ya wananchi,”amesema.
Aidha, Lupa aliwataka wakulima kujihakikishia uhakika wa chakula kwa kuhifadhi akiba ya kutosha ya chakula kipindi cha mavuno.
Kuhusu uwezo wa hifadhi ya chakula, Lupa amesema kumekuwa na ongezeko la ununuzi wa nafaka kutoka tani 58,000 hadi tani 110,000 za nafaka katika mwaka 2021/2022.
“Serikali ya awamu ya sita imeimarisha hifadhi ya chakula nchini kwa kuongeza akiba ya chakula inayohifadhiwa na wakala kwa zaidi ya mara mbili ya kipindi kilichokuwa kikihifadhiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya hivi karibuni,”amesema.
Amesema ongezeko hilo limeufanya wakala kuwa na akiba ya kutosha ya chakula kwa ajili ya kuwahudumia kwa wakati wa mahitaji mbalimbali ya dharura na upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza nchini.