WADAU wa sekta ya kilimo wameipongeza serikali kwa kuanza kutekeleza programu ya kuwezesha ushiriki wa vijana katika kilimo biashara (BBT- YIA).
Wizara ya Kilimo imeeleza kuwa programu hiyo inatarajiwa kuongeza ajira kwa vijana kufikia milioni tatu na kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
Taarifa ya wizara hiyo ilieleza kuwa inaratibu uanzishwaji wa mashamba makubwa ya pamoja na kwamba mradi huo unatekelezwa nchi nzima na vijana wote wenye sifa watapata fursa ya kufanya biashara katika mnyororo wa thamani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wizara imetambua mashamba yenye jumla ya ekari 162,492 katika wilaya za Chunya (Mbeya), Bahi na Chamwino (Dodoma), Misenyi na Karagwe (Kagera) na Uvinza na Kasulu (Kigoma).
Katika awamu ya kwanza, wizara imepanga kutoa mafunzo ya kilimo biashara kwa vijana kwa miezi mitatu katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Bihawana, Dodoma kuanzia Februari 15 mwaka huu.
Taarifa ya wizara ilieleza kuwa baada ya mafunzo, wahitimu watakabidhiwa mashamba na imekaribisha maombi ya vijana Watanzania wanaoshiriki kwenye kilimo wenye umri kuanzia miaka 18-40.
Mtaalamu wa kilimo ambaye ni waziri wa zamani wa kilimo katika serikali ya Awamu ya kwanza na ya pili, Paul Kimiti alisema programu hiyo italeta mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kuwa itaongeza viwanda ambavyo vinahitaji bidhaa za kilimo.
Kimiti alilieleza HabariLEO jana kuwa katika miaka ya 1995 hadi 1998 akiwa Waziri wa Kilimo, alitekeleza mpango unaofanana na huo kwa kutenga mashamba katika eneo linaloitwa Nyani wilayani Kisarawe.
“Tulifanikiwa kupata chakula kingi na vijana wale walifurahia mazingira ya shambani kwa sababu tuliwajali kwa kuwapa usafiri ambao tulipewa na wenzetu wa Tazara, ushirikiano mkubwa tuliopewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani wakati huo, Nicodemus Banduka,” alisema.
Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Dk Jacqueline Mkindi alisema programu hiyo ni muhimu kwa kuwa taifa lina vijana wengi zaidi kuliko makundi mengine katika jamii lakini ushiriki wao katika uzalishaji katika kilimo ni mdogo.
Dk Mkindi alisema programu hiyo itatoa fursa kwa vijana kujiajiri na kuajiri wengine kwa sababu watakapofanikiwa watasaidia vijana wengine.
“Tunaipongeza serikali kwa maono hayo kwa sababu itasaidia kwa kiwango kikubwa kuondoa vijana wengi mitaani na kusaidia kupunguza tatizo la ajira nchini, kwa hivyo malengo ya kukifanya kilimo kikue kwa asilimia 10 mwaka 2030 yatatimia kutoka hali ya sasa ya asilimia nne,” alisema Mkindi.
Alisema ni muhimu programu hiyo iwe endelevu na ili ifanikiwe, ishirikishe taasisi za fedha ili vijana wapate mitaji ya kilimo cha mashamba makubwa.
Mkufunzi Mwandamizi wa Kilimo katika Chuo cha Kilimo Tengeru Arusha, Elibariki Palangyo alisema mpango huo umefungua milango ya ajira kwa vijana na utasaidia kuondoa njaa katika jamii.
“Mpango huo utawasaidia vijana kupata pesa zitakazosaidia kunyanyua uchumi wao na familia zao pamoja na taifa kwa ujumla. Serikali pia itapata kodi kutokana na mpango huo kutokana na mpango huo kuchochea ukuaji wa viwanda,” alisema Palangyo.
Palangyo alisema programu hiyo itawasaidia pia vijana walio nje ya mpango huo kwa kupata fursa ya kufanya biashara ya pembejeo za kilimo.
Mtaalamu wa kilimo na mkulima wa mpunga mkoani Morogoro, Profesa Kitojo Wetengere alishauri programu ielimishe vijana waone umuhimu wa programu hiyo ili wawe tayari kushiriki.
“Ili kuwashawishi vijana lazima kuwe na mahala pa kujifunza hususani watu waliofanikiwa katika kilimo pamoja na kuwepo kwa miundombinu ya usafiri pamoja na kuwahakikishia soko la mazao yao watakayovuna,” alisema Profesa Watengere.
Wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema serikali inalenga kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake zaidi ya milioni tatu katika sekta ya kilimo ifikapo mwaka 2025.
“Hii itafanyika kwa kuongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 8,500,000, sawa na asilimia 50 ya eneo lote linalolimwa nchini ifikapo 2030. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itatekeleza skimu ndogo za umwagiliaji kote nchini,” alisema Dk Mwigulu.