Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaeleza zababu ongezeko bei za vyakula

BEI YA Mazao Ya Nafaka Serikali yaeleza zababu ongezeko bei za vyakula

Fri, 16 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Serikali imekiri kuwepo kwa ongezeko la bei za vyakula nchini, kutokana na upungufu wa mvua na mahitaji makuwa ya chakula ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo ya Serikali imekuja wakati kukiwa na taarifa za ongezeko la vyakula kutoka kwa wafanyabiashara.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana Desemba 15, Naibu Waziri wa wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema bei za bidhaa ya vyakula yakiwemo maharage na viazi mviringo vimepanda kutokana upungufu wa mvua.

Ametoa mfano baadhi ya vyakula ikiwemo mchele hadi kufikia Desemba mwaka huu kilo moja inauzwa kati ya Sh2,200 na Sh3,500, maharagwe yanauzwa kilo kati ya Sh2,200 hadi Sh3,650, mahindi kilo yakiuzwa kati ya Sh750 na Sh1,890 huku viazi mvirigo vikiuzwa kati ya Sh688 na 1,875 kwa kilo moja.

“Wizara hii inaratibu ukusanyaji wa taarifa za bei za bidhaa muhimu kama vile bidhaa za vyakula na vifaa vya ujenzi kupitia maofisa wa biashara mikoa na Mamlaka ya za Serikali za mitaa, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeendelea kukusanya taarifa za bei kutoka katika masoko nchini lengo la kukokotoa kiwango cha mfumuko wa bei kila mwezi,” amesema Kigahe.

Kutokana na hali hiyo amesemma Serikali inachukua hatua za dharura kukabiliana na hali hiyo kwa ikiwa pamoja na kupeleka chakula kwenye maeneo yenye uhaba.

Amekemea tabia ya baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia janga la ukame kupandisha bei za bidhaa za vyakula, akiwataka wafuate maadili ya kibiashara na ufanyaji wa biashara muda wote.

“Tunawahamasisha wenzetu wa Serikali za Mitaa wahakikishe wakulima wanapokusanya mazao yao wayapeleke sehemu husika ili wafanyabiashara hao wasiendelee kununua kwenye majumba ya watu,” amesema.

Mbali na hatua hizo, amesema pia Serikali inachukua hatua za muda mrefu ikiwa pamoja na kutengeneza miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji ili wakulima walime mazao muda wote badala ya kutegemea mvua.

Kigahe alisema ili kuleta hauweni kwa msimu wa kilimo ujao Wizara ya Kilimo imetenga zaidi ya Sh700 bilioni kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha kutoka sh 200 bilioni kwa ajili ya miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji.

“Tutahakikisha tunahamasisha vijana kulima kilimo cha biashara,” amesema.

Chanzo: Mwananchi