Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yabaini ukiritimba biashara ya sianidi

Sianidi44224f44cad2 780x470 Serikali yabaini ukiritimba biashara ya sianidi

Fri, 20 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali kupitia Ofisi ya Mkemia Mkuu imebaini uwepo wa ukiritimba wa biashara ya sianidi (Sodium Cyanide) ambayo ni mbadala wa zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu na kusababisha uhaba unaopanda gharama ya kemikali hiyo.

Mkurugenzi wa Huduma ya Udhibiti Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Daniel Ndiyo alieleza hayo mjini Geita jana alipowasilisha ripoti ya timu iliyoundwa kuchunguza uhaba wa sianidi.

Alisema uchunguzi umebaini hakuna uhaba wa sianidi bali waingizaji na wasambazaji wametengeneza uhaba na kupandisha bei kwa makusudi na wateja kushindwa kumudu gharama.

Alisema Septemba mwaka jana, kuliripotiwa uhaba mkubwa wa sianidi nchini na kuanza kuuzwa kwa Sh milioni 1.2 sawa na mara tatu ya bei ya awali ambayo ilikuwa ni Sh 400,000 kwa pipa la kilo 50.

Daniel alisema ofisi ya mkemia mkuu wa serikali ilifanya kikao na tume ya madini, waingizaji, wasambazaji na watumiaji wa sianidi na kuazimia bei elekezi isizidi Sh 600,000 kwa pipa la kilo 50.

“Timu imebaini baadhi ya waingizaji na wasambazaji bado wanauza sianidi kwa bei ya Sh 800,000 hadi 950,000 na kutokana na hilo, tayari hatua zimeshachukuliwa kwa wahusika,” alisema.

Alitaja kampuni sita za wasambazaji na mtu mmoja wamepigwa faini ya Sh milioni 61 ambao ni Jacho Chemical Ltd, Oxley Ltd, Cavibou first Ltd, Jema Chemical Limited, ETG Curechem Ltd, Mayengo Trading Company Ltd na Juma Sultan.

Alisema ili kudhibiti ukiritimba, wateja na wasambazaji wameagizwa kujisajili ofisi ya GCLA na kuwasilisha taarifa za mauzo kila siku kubainisha kiasi gani kimeuzwa, kwa nani na kiasi kilichobaki.

Meneja Ukaguzi Migodi kutoka Tume ya Madini, Winnifida Mrema alikiri uhaba wa sianidi umesababisha kushuka kwa uzalishaji wa dhahabu kutokana na wachimbaji wengi kushindwa kumudu gharama kubwa ya kemikali hiyo ya uchenjuaji.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella aliahidi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia, kuwakamata na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote watakaokiuka utaratibu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live