Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaamsha sekta binafsi kupaisha kilimo

603225bef0fb7d97efe093a199bd33b2.jpeg Serikali yaamsha sekta binafsi kupaisha kilimo

Mon, 20 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Serikali imeitaka sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuwezesha sekta ya kilimo kuchangia zaidi pato la taifa kwa kuinua kilimo cha mtu mmoja mmoja, badala ya kusubiri matamko ya serikali.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kaspar Mmuya wakati akizungumza na wadau mbalimbali katika warsha ya mapitio ya wadau kwenye rasimu ya taarifa ya tathmini jumuishi ya sekta ya kilimo mwaka 2017-2020 mwishoni mwa wiki.

Akizungumza katika warsha hiyo iliyofanyika Dar es Salaam, Mmuya alisema awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inataka sekta binafsi kusisimua uchumi kwa kushiriki kikamilifu katika sekta ya kilimo ambayo ni mtambuka.

“Tumezungumzia serikali iweke nafasi kwa sekta binafsi… serikali haijazuia nyie kuwatambua na kuwekeza katika uelewa, uwezo wa watu, mkawapa fedha, mkawasimamia na kuhakikisha kwamba yanapatikana matokeo makubwa katika kilimo,”alisema Mmuya.

Alisema pamoja na kwamba Azimio la Malabo linataka kilimo kiwe kinapata asilimia 10 ya bajeti ya nchi, kutokana na uhaba wa rasilimali fedha ni vyema sekta binafsi ikahakikisha inabuni na kutekeleza mipango inayoweza kuwa na mchango mkubwa katika sekta ya kilimo, kwa kuwatambua watu ambao wanaweza kutumika kama mfano, hivyo kusisimua uchumi na ajira. Akizungumzia utafiti alisema, “Vituo vya utafiti na nyie watafiti zile zilizopo zimetumika kiasi gani?

Hizi tafiti zimetumika katika nini, zimeleta mabadiliko gani? Tumeomba fedha kutoka kwa watu mbalimbali na tumepata, tumefanya tafiti, nini matokeo yake?”

Akiwasilisha mada kuhusu tathmini ya umma kwenye sekta ya kilimo, mmoja wa washauri katika utafiti huo, Omar Selemani akishirikiana na Dk Hussein Nassoro walisema kwamba kuna pengo kubwa la rasilimali fedha linalofanya kilimo kisikue.

Alisema kwa sasa bajeti ya kilimo ni asilimia 2.9 kwa mwaka 2019/2020 ikiwa haiongezeki kwa muda mrefu huku mchango wa kilimo katika pato la taifa ukibaki asilimia 3.9 karibu sawa na bajeti yake kwa mwaka 2019/2020.

Ingawa bajeti ya kilimo imeongezeka kutoka Sh bilioni 585 mwaka 2017/18 na kufikia bilioni 970 kwa mwaka 2019/2020 umaskini unaongezeka huku kundi la wakulima likiendelea kuongezeka na hivyo kutoa ishara hasi kwa uchumi wa taifa na maendeleo yake.

Pamoja na kukiri kuwa kuna kiasi kidogo cha fedha, Mmuya alisema ni lazima wataalamu kutumia rasilimali zilizopo kuleta mabadiliko ikiwamo kuheshimu elimu ya wazawa na ile waliyoikuta ili kuwafanya wananchi kulima kisasa zaidi na kuwa na mchango mkubwa katika uchumi. Alisema mifumo iliyopo ya ukusanyaji wa takwimu na tafsiri zake ni lazima ifanyike kwa pamoja na kushirikishwa taasisi ya mifumo ya serikali IGA kwa matokeo makubwa badala ya kila mtu kufanya chake na kuondoka ikiwa hakiendelezwi.

Katika warsha hiyo ambapo pia washiriki wengine waliohudhuria kwa kutumia video, mawasilisho matatu yalifanyika yaliyolenga kuangalia changamoto na mapendekezo ya kuondokana na changamoto hizo katika kilimo na kukifanya kwua cha kisasa na cha kibiashara.Mawasilisho hayo yaliyotokana na utafiti uliofanywa na kundi la wataalamu 25 kuhusu sekta ya kilimo kama nyenzo ya uwajibikaji kwenye makubaliano ya kikanda (CAADP), Tathmini ya matumizi ya umma kwenye sekta ya kilimo na tathmini ya sekta ya kilimo ualilenga kuona changamoto katika utekelezaji wa ASDPII na uoanishaji wa mafanikio na changamoto katika mpango wa maendeleo wa taifa.

Mawasilisho hayo yalifanywa na Stella Clara Masawe kutoka AGRA, Omar Selemani na Dk Hussein Nasoro, Profesa Deogratius Mushi kutoka Shule ya Uchumi UDSM na Profesa Beatus Kundi ambao walishiriki utafiti huo.

Kauli zingine zilitoka kwa mchumi wa Benki ya Dunia, Emma Isinika na mtaalamu wa kilimo mstaafu aliyewahi kuwa Katibu Mkuu, Peniel Lyimo ambaye alisema kilimo ni sayansi na huwezi kukwepa mchakato wake hivyo kinafaa kuangaliwa zaidi katika mipango ya muda mrefu Mchumi wa Benki ya dunia alisifu kikao hicho kwani alisema kitatoa taarifa ya hali halisi, mwelekeo na nini hasa kinafaa kufanyika ili kuleta maendeleo yaliyokusudiwa katika sekta ya kilimo ambayo ndiyo inayotegemewa na wengi katika vita dhidi ya umaskini.

Naye mwakilishi mkazi wa AGRA, Vianey Rweyendela, alisema tafiti hizo na ripoti zake zitasaidia sana kuboresha mifumo iliyopo ili iweze kukiendeleza kilimo na kuwa cha kisasa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz