Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali yaahidi kutatua changamoto zote za startups Tanzania

Nalani.jpeg Mwigulu akiwa na mjasiriamali wa Kitanzania Benjamin Fernandes

Wed, 20 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imewataka vijana wa Tanzania kuchangamkia fursa za maendeleo ya Tehama ili waweze kujikwamua kiuchumi huku akiahidi kutatua changamoto zinazowakabili wakati wakiendesha kampuni chipukizi (startups).

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, aliyekuwa akizungumza Aprili 18, 2022 New York, Marekani wakati alipozindua programu tumishi ya NALA (NALA App) itakayotumiwa na Watanzania waishio Marekani kutuma fedha Tanzania kidijitali ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazozikabili startups ikiwemo upatikanaji wa leseni za kuendesha shughuli zao.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuwatia moyo vijana wabunifu wawekeze kwenye mifumo ya kidijitali inayoweza kuchangia ukuaji wa matumizi ya teknolojia katika kuongeza kipato cha wananchi na Taifa kwa ujumla.

​“Nimefahamishwa kwamba Marekani imewekeza karibu Dola bilioni 1.5 (Sh3.5 trilioni) katika Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Barani Afrika, ninatamani kuona kuwa Tanzania inakuwa ni moja ya nchi zitakazonufaika na uwekezaji huo,” amesisitiza Dk Nchemba katika hotuba yake akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya Tehama kwa kujenga mkongo wa Taifa uliounganishwa na nchi nyingine za Afrika zikiwemo Burundi, Rwanda, Kenya, Malawi, Uganda na Zambia na hivi karibuni nchi za DRC na Msumbiji zitaunganishwa.

Amewaomba wawekezaji kwenye sekta ya Tehama kuwekeza nchini Tanzania na kufaidi mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo nchi imeweka ili kuvutia mitaji na teknolojia.

Akizungumzia programu ya NALA, amesema inarahisisha utumaji wa fedha kutoka nchini humo kwenda Tanzania hatua ambayo itasisimua uchumi wa nchi na kuharakisha maendeleo ya wananchi watakaofaidika na huduma hiyo.

“Benjamin Fernandes na timu yako ni miongoni mwa vijana wabunifu waliojikita katika masuala ya teknolojia ambao Serikali inawaunga mkono hususan wakati huu ambapo nchi inajenga uchumi wa kidijitali ambao matokeo yake yanatarajiwa kuwa ni kukuza ajira, kuchangia pato la Taifa na kukabiliana na changamoto zote za kiuchumi na kijamii,” amesema Dk Nchemba.

Programu ya NALA inawawezesha watu kufanya miamala ya kifedha kwa kutumia programu ya simu (App) wakiwa popote bila kusubiri muunganiko wa mtandao wa intaneti au kupanga foleni benki na kwenye vibanda vya kutolea pesa.

Pia inawawezesha kulipia huduma za makampuni kwa kutumia simu ya kawaida au simu janja.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Benjamin Fernandes amesema kuwa programu hiyo iliyozinduliwa nchini Marekani, inafanya kazi katika nchini nyingine tisa duniani na aliibuni kwa ajili ya kusaidia utumaji wa fedha kwa nchi za Afrika.

Aidha, Fernandes aliiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza masharti ya leseni ya biashara ya mitandao ili kuwawezesha vijana wengi wabunifu wa Tehama, kuwekeza nguvu zao kwa kuwa itaongeza ajira na kukuza uchumi wao.

Amesema kuwa hivi sasa mtu anayetaka kutoa huduma za kifedha za kibunifu analazimika kulipia leseni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hata bila kuanza kufanya kazi hatua ambayo amesema inawakwaza vijana wengi kutimiza ndoto zao za kujiajiri na kuwaajiri watu wengine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live