Handeni. Naibu Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Subira Mgalu amesema hakuna utaratibu wa wananchi kuuziwa nguzo wanapohitaji kuunganishiwa umeme majumbani.
Akizungumza leo Alhamisi Novemba 21, 2019 na wakazi wa mtaa wa Komwale halmashauri ya mji Handeni, Mgalu amewataka kuripoti katika vyombo vya usalama ikiwa watauziwa nguzo.
Amesema wanatakiwa kutoa Sh27,000 tu kwa ajili ya kuunganishiwa nishati hiyo na si kulipia nguzo.
“Hatufanyi mchezo na maelekezo ya Rais John Magufuli namtafuta huyo anayesema kuwekewa umeme mwananchi bila kulipia nguzo haiwezekani. Ndani ya saa 24 hatakuwepo maana nitashughulika naye,” amesema Mgalu.
Amesema kuunganishiwa umeme si anasa bali kukuza uchumi wa nchi na wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe amesema ujio wa Mgalu wilayani humo umesaidia kupatikana vituo viwili vya kupoza umeme eneo la Mkata na Handeni mjini.
Meneja Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Tanga, Julius Sabu amesema wameshaanza utaratibu kwa ajili ya kufunga vituo vya kupooza umeme eneo la Mkata na Handeni mjini kwa ajili ya kutatua changamoto ya kukatatika umeme.