Rukwa. Wasafirishaji wa mizigo wa ndani na nje ya Tanzania katika ukanda wa ziwa Tanganyika wanasema endapo Serikali ya nchi hiyo itaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya bandari, reli na barabara biashara ya usafirishaji katika maeneo hayo itakuwa vizuri.
Jana Jumamosi Desemba 21, 2019 Mwananchi ilifika katika bandari ya Kasanga na kukuta meli moja ya MV Rwegura kutoka nchini Burundi, yenye uwezo wa kupakia tani 500 ikiwa inapakia Saruji na nahodha wa meli hiyo Bonyumuvunyi Michael alisema kwa sasa huo ndiyo mzigo pekee unaochukuliwa katika bandari hiyo.
”Mara nyingi meli hii ikija Tanzania inakuwa imefuata saruji Kasanga au mizigo mingine kigoma, biashara inakwenda vizuri maana mpaka sasa nishafanya safari 27 katika mwaka huu lakini biashara itakuwa vizuri Zaidi tukiwa tunapata mzigo wa kuja huku,” alisema.
Alisema meli kama ilivyo vyombo vingine vya usafiri inakuwa na faida kama kuna mizigo ya kwenda na kurudi hivyo maboresho katika bandari za Tanzania na njia nyingine za usafiri zitasaidia kuboresha biashara yao.
“Kwetu bidhaa tunayouza nje sana ni chai na kahawa, awali zilikuwa zinasafirishwa kwa meli mpaka Kigoma kisha Dar es Salaam kwa treni lakini hapo katikati treni haikufanya vizuri watu wakaamua kuanza kutumia barabara (malori) ili kuwahisha mizigo yao,” anasema.
Alisema kama usafiri wa treni utakuwa wa uhakika na bandari zikaruhusu meli kubwa tofauti kutia nanga basi biashara hiyo itarejea tena kwa kasi.
Yusuph Robert Dereva wa lori linalosafirisha saruji ya Mbeya Cement alisema ujenzi wa barabara ya lami kumpunguzia muda wa safari kutoka siku saba au zaidi hadi siku moja kwa safari ya kutoka Mbeya kwenda bandari Kasanga kupitia Sumbawanga.
“Hivi sasa baada ya njia yote kuwekwa lami nikitoka Mbeya kwenda Kasanga (Takribani Kilometa 430) natumia siku moja kufika bandarini na kesho yake nashusha kisha nageuka lakini zamani ilikuwa ni safari ya siku saba hata wiki mbili barabara ikiwa na utelezi,” alisema.
Alisema safari ya kutoka Sumbawanga mjini hadi bandari ya Kisanga ilikuwa inachukua wastani wa siku mbili wakati umbali wake ni wastani wa Km100.
“Nasema wakati huo posho ya safari ilikuwa haina thamani tena kwakuwa wakati mwingine yote iliishia njiani lakini hivi sasa mambo ni mazuri mzigo unafika haraka mtu anawahi kufanya safari nyingine,” alisema
“Tatizo tu ni kwamba bandari haijachangamka sana sie tunapeleka mizigo lakini hatupati wa kurudi nao hivyo magari yanarudi matupu, Serikali inaweza ikaangalia namna ya kutatua hilo maana tukipata mizigo ya kurudi matajiri watapata fedha nasi tutaongezewa posho,” alisema.
Aidha Meneja wa bandari za ziwa Tanganyika, Percival Salama alisema Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inatekeleza mradi wa Sh4.76 bilioni kwa ajili ya kuboresha bandari ya Kasanga ambayo aliitaja kuwa ni ya kimkakati kwakuwa ina uwezo wa kuhudumia nchi nyingi kwa urahisi.
Alisema mradi huo wa miezi 12 ulianza Aprili 29, 2019 na hivi sasa umekamilika kwa asilimia 25, unahusisha upanuzi wa gati kutoka mita 20 hadi 120 ili kuruhusu meli za ukubwa tofauti, jengo la kupumzika abiria na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi.