Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Tanzania yapokea Sh1.05 trilioni za gawio, michango

85654 Pic+waziri+mpango Serikali ya Tanzania yapokea Sh1.05 trilioni za gawio, michango

Sun, 24 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Philip Mpango amesema mapato ambayo yanatokana na gawio na michango ya kampuni, taasisi na mashirika imeongezeka kutoka Sh162.04 bilioni mwaka 2014/15 hadi kufikia Sh1.05 trilioni kwa mwaka 2018/19.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2018/19 makusanyo ya mapato yanayopita katika akaunti ya msajili wa hazina yamevuka lengo kwa kukusanya kiasi cha Sh683.23 bilioni sawa na asilimia 114.3 ikilinganishwa na malengo ya Sh597.7 bilioni.

Waziri Mpango amesema hayo leo Jumapili Novemba 24, 2019 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kupokea gawio na michango kutoka katika taasisi, mashirika na kampuni ambazo serikali ina hisa.

Amesema mapato hayo yanajumuisha mapato yaliyokusanywa  kupitia akaunti zilizopo chini ya msajili wa hazina ambazo zilileta Sh683.23 bilioni fedha zilizopelekwa moja kwa moja mfuko mkuu wa Serikali kutoka taasisi na Wakala wa Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) na Bodi ya  Michezo ya Kubahatisha.

“Mafanikio hayo yametokana na sera na usimamizi bora  wa rasilimali za serikali  ikijumuisha kuongezeka kwa mashirika yanayotoa gawio na michango, kuimarisha ufuatiliaji na uchambuzi wa mashirika hayo ili kuhakikisha yanaongeza ufanisi pamoja na ufuatiliaji na udhibiti wa matumizi uchambuzi wa bajeti na hesabu,” amesema Waziri Mapngo.

Waziri Mpango amesema usimamizi wao katika masuala ya kisera kwa taasisi na mashirika haya ndio umechangia kupatikana kwa mafanikio hayo.

“Kwa hakika bila michango hii na fedha ambazo zitakabidhiwa leo kwa hundi ya mfano mimi siwezi kuwa kazini maana ni moja ya majukumu ya msingi ambayo umenipa,” amesema

Aidha amewashukuru mawaziri kutoka wizara mbalimbali kwa  ushirikiano wao lakini pia ofisi ya msajili wa hazina kwa kusimamia na kutekeleza majukumu ya taasisi, wakala na mashirika ambayo yapo chini ya wizara zao.

“Nashukuru pia kamati ya Bunge ya uwekezaji wa mitaji ya umma, imekuwa ikitupatia ushauri na maelekezo ambayo imetusaidia kuimarisha usimamizi na utendaji wa taasisi za umma lakini pia mdhibiti  na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali, Charles Kichere katika siku chache ambazo amekuwepo ofisini tayari ameshaanza kutuwashia cheche kuhakikisha kuwa taasisi hizi hazizembei tena kuwasilisha gawio na mapato mengine serikalini kama inavyostahili kwa mujibu wa sheria,” amesema Waziri Mpango

Chanzo: mwananchi.co.tz