Dodoma. Serikali imelazimika kutoa ufafanuzi bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Mei 30, 2019 kuhusu ucheleweshaji wa safari za ndege ikibainisha kuwa jambo hilo linashughulikiwa.
Ufafanuzi huo umetolewa na naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye akifafanua kuwa ucheleweshaji ulikuwa katika Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Nditiye alikuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aliyehoji sababu za ndege kuchelewa kuanza safari na wakati mwingine taarifa haitolewi kwa abiria.
“Kumekuwa na ucheleweshaji wa safari za ndege na muda husogezwa na wakati mwingine bila taarifa sahihi, nini kinachangia jambo hili,” amehoji Nape.
Naibu Waziri huyo amesema wamefanya mabadiliko makubwa ATCL hivyo abiria kuchelewa kumepungua na ikitokea taarifa hutolewa mapema.
Katika swali la msingi mbunge wa Shaurimoyo (CCM) Mattar Ali Salum amehoji kama Serikali inajua kero wanazopata abiria katika kampuni ya Azam Marine, kwa maelezo kuwa mtu akichelewa hata tiketi aliyonayo haiwezi kuitumia tena.
Pia Soma
- UCHOKOZI WA EDO: STK na STL zinaweza kushiriki Formula One
- Nyalandu azungumzia uchafu mahabusu
- Serikali yatangaza fursa mpya mifuko ya plastiki
Hata hivyo, Nditiye amesema abiria watakaochelewa wakitoa taarifa mapema hawatozwi gharama zozote.