Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano nchini Tanzania, Atashasta Nditiye ameionya kampuni ya simu ya Halotel nchini kuacha kutumia mkongo wa Taifa wa mawasiliano kupeleka mawasiliano nje ya nchi.
Nditiye ametoa kauli baada ya kubaini kampuni hiyo inapeleka mawasiliano yake kutoka Tanzania kwenda Burundi kwa kuunganisha jozi za mawasiliano za kampuni hiyo kwenye mfumo wa mkongo wa Burundi badala ya kufanya maunganisho huo kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (Nictbb).
Nditiye ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Oktoba 7,2019 katika ziara ya kukagua miundombinu na mwingiliano wa mawasiliano kati ya Kabanga mpakani mwa Tanzania na Burundi.
Nditiye ametoa kauli hiyo baada ya kufika katika maunganisho ya mkongo wa Taifa wa mawasiliano unaotumika kupeleka mawasiliano kutoka Tanzania kwenda nchi jirani.
“Nawaelekeza Halotel watumie mkongo wa Taifa wa mawasiliano kupeleka mawasiliano nchi jirani ili kufuata utaratibu uliowekwa baina ya nchi moja na nyingine wa kuvusha mawasiliano yake kwenda nchi jirani,” amesema Nditiye.
Nditiye amesema Halotel hawaruhusiwi kufanya hivyo, akibainisha kuwa wanakiuka utaratibu na wanaikosesha nchi mapato sambamba kuhatarisha usalama wa Taifa kwa kuwa hakuna atakayeweza kufuatilia mawasiliano upande wa pili wa nchi hiyo.
Pia Soma
- Profesa Kabudi ataja sababu kuambatana na Magufuli
- VIDEO: Warioba: Vita ya rushwa inakwepa viongozi
- Huduma za kidijitali NMB sasa kwa Kiswahili
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Michael Mntenjele amesema wilaya inahitaji mawasiliano ya uhakika na yasiyokuwa na msongamano ili kufanikisha suala la ulinzi na Usalama wa Taifa.