Dodoma. Serikali ya Tanzania itaendelea kuvutia uwekezaji katika maeneo yote yenye rasilimali ikiwemo Jasi inayopatikana katika kata za Bendera na Makanya wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu Februari 3, 2020 na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angella Kairuki wakati akijibu swali la Mbunge wa Same Mashariki (Chadema) Naghenjwa Kaboyoka.
Kaboyoka amesema kata za Bendera na Makanya zina Jasi nyingi na zinaweza kutoa malighafi kutengenezea Gypsum boards, mabomba ya maji machafu, saruji, POP na mbolea.
“Serikali ina mpango gani wa kusaidia kupatikana kwa
mwekezaji ili aanzishe viwanda hivyo katika maeneo hayo wilaya ya Same,” amehoji.
Akijibu swali hilo, Kairuki amesema azma ya Serikali ni kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025.
Pia Soma
- VIDEO: MWANZO, MWISHO VIFO WATU 20 KONGAMANO LA MWAMPOSA
- Waliofariki kongamano la Mtume Mwamposa kuagwa leo
- VIDEO: Rais Magufuli awaapisha viongozi aliowateua
Amesema viwanda vinavyotumia rasilimali zinazopatikana nchini na kuzalisha bidhaa zinazotumika kwa wingi vimepewa kipaumbele.
“Kutokana na utekelezaji wa azma hiyo, nchi yetu sasa imeweza kuzalisha baadhi ya bidhaa zinazotosheleza soko la ndani na ziada kuuza nje ya nchi ikiwemo bidhaa zinazotokana na malighafi ya jasi,” amesema.
Amesema lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje katika maeneo yote yenye rasilimali zinazoipa Tanzania faida ya ushindani.