Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema imepata taarifa za notisi ya kutaka kufungwa kwa baadhi ya viwanda vinavyotumia gesi asilia ila inachukua hatua kunusuru hali hiyo.
Hayo yamesemwa na naibu waziri wa nishati, Subira Mgalu alipokuwa akijibu swali la Rashid Akbar, Mbunge wa Newala Vijijini aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuongeza tija kwenye sekta hiyo.
"Serikali imepokea taarifa hizo na inazifanyia kazi. Jukumu la kupanga bei ya nishati nchini lipo chini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (Ewura) mbayo inashirikiana na Mamlaka ya Mkondo wa Juu wa Mafuta (Pura)," amesema Mgalu.
Serikali imetoa majibu hayo bungeni leo Jumanne Aprili 30 na kueleza kuwa inaendelea kuboresha mazingira ili kuwavutia wawekezaji wa kutumia gesi asilia.
Kwenye swali lake la nyongeza, Akbar alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kuviokoa viwanda vinavyotumia gesi hiyo ambavyo vimepewa notisi ya kufungwa kutokana na kupokea kiasi kidogo cha nishati hiyo kuliko mahitaji yao.
Licha ya kiwango kidogo, Akbar alihoji suala la bei akieleza kuwa wateja nchini wanalipa Dola 5.5 za Marekani kwa kila tani moja ya ujazo ilhali bei ya dunia ni Dola tatu tu kwa kiasi hicho.
Kwenye majibu yake, naibu waziri amesema uzalishaji wa nishati hiyo nchini unagharimu Dola 5.36 za Marekani, hivyo kulazimu kuiuza kwa bei hiyo.
"Wawekezaji wengi wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea. Serikali inaendelea kuwakaribisha wawekezaji kutoka popote walipo," amesema Mgalu.
Kwenye swali la msingi, Akbar aliuliza kwa nini kiwanda cha Dangote hakijaunganishwa na gesi asilia na kwa nini wananchi wa Mtwara hawatumii gesi asilia kwenye nyumba zao.
Akijibu, Mgalu alisema Serikali imeshakiunganisha kiwanda cha Dangote tangu Agosti mwaka jana na mpaka sasa kinatumia kati ya futi milioni 15 hadi 20 za ujazo kwa siku na kwamba miradi wa kuunganisha kiwanda hicho umegharimu Sh8.2 bilioni.
Mpaka Juni mwaka huu, Mgalu amesema nyumba 120 mkoani Mtwara zitakuwa zimeunganishwa na gesi asilia ikiwa ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo.