Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Tanzania kuwekeza maeneo yasiyo na mawasiliano

Serikali ya Tanzania kuwekeza maeneo yasiyo na mawasiliano

Fri, 1 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema iko tayari kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya kushirikiana na wadau wa mawasiliano kuelekeza nguvu zote kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na mawasiliano.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Oktoba 30, 2019 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako aliyemwakilisha Waziri Mkuu kufungua kongamano la nne la mitandao jamii.

“Serikali iko tayari kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wote wanaoshiriki katika jitihada za kuimarisha mawasiliano kwa wote hususan kuelekeza nguvu zetu zote katika maeneo ambayo bado hayajafikika,” amesema.

Amesema licha ya jitihada zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau kuimarisha mawasiliano, lakini bado kuna umuhimu wa kuongeza fursa ya kuunganisha nguvu na wadau ili kuboresha hali ya mawasiliano nchini.

“Wadau (wa mawasiliano) ni muhimu sana katika kufanikisha azma ya Serikali lakini pia azma ya muungano wenu wa huduma za mtandao jamii katika kuhakikisha kuwa tunaunganisha watu ambao hawajaunganishwa,” amesema.

Mwakilishi wa Shirika linalojihusisha na Mtandao la APC, Dk Carlos Rey-Moreno amesema utafiti uliofanywa na Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Jebhera Matogoro unaonyesha Televisheni ndiyo suluhisho linaloweza kutumika kuunganisha watu wanaoishi vijijini. Matogoro amesema utafiti huo alioufanya Wilayani Kondoa mkoani Dodoma umelenga kuwawezesha wakazi wa vijijini kupata huduma ya mtandao kwa kutumia mawimbi ya Televisheni.

Kongamano hilo limeandaliwa na Shirika la Internet Society, APC na Udom na kuwashirikisha washiriki 100 kutoka ndani na nje ya nchi.

Chanzo: mwananchi.co.tz