Mtwara. Waziri wa Kilimo, Japheth Hasunga ameanza kazi kwa kishindo akibainisha kuwa wakulima wa korosho wataanza kulipwa kuanzia kesho Jumatano Novemba 15, 2018.
Hasunga aliyeteuliwa Novemba 11, 2018 kuchukua nafasi ya aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Charles Tizeba ambaye uteuzi wake ulitenguliwa ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 13 mkoani Mtwara katika mkutano wake na wanahabari baada ya kufanya kikao na mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Glesius Byakanwa.
"Tunataka kuanzia kesho wakulima wapewe fedha zao, tumeshaandaa fedha zipo," amesema Hasunga.
Amesema licha ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo kutokuwa na matawi mikoani, wakulima watapewa fedha kupitia akaunti za benki wanazohudumiwa au kwa hundi.
"Serikali tunatamani kila mkulima apewe fedha zake, lakini akipewa fedha taslimu kama Sh5 milioni inaweza kuwa hatari kiusalama. Lakini nimeambiwa kila mkulima ana akaunti ya benki," amesema.
Kuhusu bei, Hasunga amesema iliyopangwa na bodi ya korosho haitatumika na kwamba hata ya Sh3,300 watakayonunulia haitatumika kukokotoa makato ya mkulima, bali watafanya tathmini na kukata makato baadaye.
"Tunachotaka wakulima wapate fedha kwanza," amesisitiza.
Huku akiwa ameongozana na naibu wake, Innocent Bashungwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mathew Mtigumwe, waziri huyo ametaja malengo matatu ya ziara hiyo kuwa ni pamoja na kuhakiki wingi wa korosho iliyopo.
Amesema wamelenga kuangalia ubora wa maghala yaliyopo na ukubwa wake.
"Tunataka kujua hata maghala yanamilikiwa na nani!? Je ni watu binafsi, bodi au vyama vya ushirika?" amehoji.
Kuhusu ubanguaji wa korosho, Hasunga amesema mkakati uliopo ni kuzibangua korosho zote na kuziuza nchini.
Awali wakitoa takwimu, kaimu mrajisi wa ushirika mkoani hapa, Salum Issa amesema chama cha ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu) kina jumla ya tani 3, 563, 465 huku mwakilishi wa chama cha Masasi na Mtwara (Mancu), Potency Rwiza akisema kina jumla ya tani 35,043,055.