Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Tanzania imetangaza kutonunua korosho msimu ujao

74584 Korosho+pic

Sat, 7 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali ya Tanzania imetangaza kutonunua korosho katika msimu ujao wa mavuno na badala yake itasimamia utaratibu wa ununuzi huo usimuathiri mkulima.

Hayo yamesema bungeni leo Ijumaa Septemba 6, 2019 wakati Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Newala Vijijini (CCM) Rashid Ajali.

“Serikali ina mpango gani juu ya msimu wa korosho ambao umebaki miezi mitatu ili kuepuka mgogoro uliojitokeza mwaka jana. Ili bei ya korosho ibaki kati ya mkulima pamoja na mfanyabiashara,” amehoji Ajali.

Akijibu swali hilo, Bashe amesema wiki ijayo Waziri wa Kilimo Japheth Hasunga atatangaza utaratibu utakaotumika katika ununuzi wa korosho katika msimu ujao.

“Tumeamua na wiki ijayo, Waziri wa Kilimo atatangaza hadharani utaratibu na namna gani mfumo wa korosho utakavyokuwa, lakini mfumo ujao wa ununuzi wa korosho utakuwa ni mfumo wa wafanyabiashara kununua korosho na Serikali itakuwa pale kuangalia utaratibu ule hamuathiri mkulima,” amesema.

Amesema Serikali itatangaza utaratibu wa kutangaza zabuni kwa uwazi na hawatatumia utaratibu wa viboksi wa watu usiku wa manane kwenda kutengeneza  ushawishi (cartel) ambao siku ya mwisho utakwenda kutuletea matatizo.

Pia Soma

Advertisement
Amesema uwazi ndio utakuwa msingi wa ununuzi wa zao la korosho na kwamba matatizo yaliyojitokeza katika msimu uliopita hayatajitokeza tena. 

Katika swali la msingi, Ajali alihoji Serikali imejiandaaje ili kuwapatia wakulima wa korosho pembejeo za uhakika na kwa wakati.

Akijibu, Bashe amesema Serikali kupitia Bodi ya Korosho imeweka utaratibu wa kuwakopesha wakulima pembejeo hizo kupitia vyama vya msingi vya Ushirika (AMCOS) ili kurahisisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati.

Aidha, amesema Serikali kupitia Taasisi ya Viuatilifu (TPRI) inaendelea kukagua ubora wa viatilifu katika maduka na maghala ya wafanyabiashara kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanapata viatilifu vyenye ubora.

Chanzo: mwananchi.co.tz