Dar es Salaam. Baada ya mgogoro uliodumu tangu mwaka 2017, Kampuni ya Barrick na Serikali zimeunda kampuni ya Twiga itakayosimamia migodi mitatu iliyokuwa chini ya kampuni ya Acacia.
Kwenye kampuni hiyo mpya, Barrick itamiliki asilimia 84 ya hisa zote huku Serikali ikiwa na asilimia 16. Utaratibu huo ni utekelezaji wa sheria mpya ya madini iliyopitishwa mwaka 2017.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Profesa Palamagamba Kabudi amesema ‘sasa amezaliwa mtoto mpya baada ya Barrick kukubali kumuua mtoto wake, Acacia.’
Mgogoro kati ya Serikali na kampuni ya Acacia iliyokuwa inasimamia migodi ya Buzwagi, North Mara na Bulanhulu ulianza mwaka 2017 na Rais John Magufuli akaunda tume ya kuchunguza mwenendo wa biashara ya madini.
Tume hiyo ilibaini ukiukwaji wa sheria, utaratibu na kanuni zilizopo hivyo kuikosesha Serikali mapato inayostahili. Kutokana na hilo, Serikali iliipiga faini ya Dola 190 bilioni jambo lililosababisha kuanza kwa mzungumzo baina ya pande hizo mbili.
Kwenye mazungumzo hayo, Acacia ambayo ni kampuni tanzu ya Barrick iliwekwa pembeni na majadiliano yakafanywa na Barrick…mwisho wa siku, Acacia imefutwa sokoni na badala yake, Twiga itachukua nafasi yake.
Pia Soma
- Rais Magufuli kuwaapisha watendaji aliowateua jana muda mfupi ujao Ikulu
- Ndani ya boksi: Katikati ya Mondi na Kiba kuna fursa hii
- Jinsi Awadh alivyoyapigania maisha akitumia mtungi wa oksijeni