Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali, wadau wahitimisha sakata la uhaba wa saruji

12311 Pic+saruji TanzaniaWeb

Fri, 17 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imekubaliana na wadau wa saruji kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana sokoni kwa uhakika na bei ishuke ndani ya wiki moja.

Pia, wamekubaliana kampuni ya Tancoal ambayo ni wazalishaji wakuu wa makaa ya mawe wahakikishe yanapatikana kwa wingi kwa viwanda vya ndani kabla ya kuuzwa nje.

Imeelezwa upatikanaji mdogo wa makaa ya mawe ni chanzo cha uhaba wa saruji nchini, jambo lililosababisha kuadimika kwa bidhaa hiyo na kupanda bei sokoni.

Hayo yamebainishwa wakati wa kikao cha pamoja kati ya Serikali ikiwakilishwa na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya na wadau wa uzalishaji wa saruji wakiwamo wazalishaji wa saruji, makaa ya mawe, wasafirishaji na wadhibiti.

Akizungumza baada ya majadiliano yaliyofanyika juzi jijini Dar es Salaam, Manyanya alisema wamebaini kuna mahitaji makubwa ya makaa ya mawe na saruji ndani na nje ya nchi.

“Tumekubaliana Tancoal atahakikisha makaa ya mawe yanapatikana kwa wingi kwa viwanda vya ndani kabla ya kuuzwa nje. Lazima tujifikirie sisi kwanza, tukitosheka na mahitaji basi ile ziada ndiyo tuuze nje,” alisema.

Naibu waziri huyo alisema uhaba wa saruji pia umesababishwa na changamoto ya usafirishaji.

Alisema malori yanayosafirisha makaa ya mawe kutoka migodini hutumia muda mrefu njiani kutokana na miundombinu mibovu ya barabara.

Changamoto nyingine, alisema ni kuharibika kwa mitambo.

Wazalishaji saruji walimhakikishia naibu waziri kuwa baada ya wiki moja uzalishaji utarejea katika hali ya kawaida.

“Tunatarajia ndani ya wiki moja upatikanaji wa saruji utarejea katika hali ya kawaida. Natoa rai kwa wote wanaouza saruji kwa bei ya juu warudishe bei za kawaida, vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema naibu waziri.

Aliwataka wazalishaji wa saruji kutumia miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali kama fursa ya kuuza bidhaa yao kwa sababu mahitaji ni makubwa na soko ni la uhakika.

Pia, aliwataka waongeze uzalishaji ili kufaidi soko hilo.

Walichosema wadau

Akizungumza na Mwananchi baada ya kikao hicho, Meneja Mitambo wa Kampuni ya Saruji Tanga, Benedict Lema alisema kiwanda chao kinahitaji tani 600 za makaa ya mawe kwa siku, lakini kinapatiwa tani 300.

Lema alisema wakipata kiasi wanachohitaji watazalisha tani 4,000 za saruji kwa siku.

Alisema mahitaji ya saruji kutoka kiwanda hicho yamekuwa makubwa zaidi baada ya kufungwa viwanda vya Twiga na Dangote.

“Mitambo yetu haijapata matatizo, vinu namba moja na mbili vyote vinafanya kazi vizuri. Changamoto ilikuwa tunapata malighafi kidogo,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Twiga, Alfonso Velez alisema kilifungwa kwa sababu ya matatizo ya kiufundi, lakini siku tatu zilizopita wameanza kurudi kwenye hali ya kawaida ya uzalishaji.

Kuhusu uzalishaji wa makaa ya mawe, Alex Rutagwelela, kaimu mkurugenzi wa utafiti na uchorongaji wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico), alisema kuanzia Mei, 2017 walipoanza uzalishaji, wanazalisha tani 8,600 kwa mwezi.

Alisema wanatarajia kuzalisha tani 18,000 kwa mwezi kuanzia Septemba katika mgodi wao wa Kiwira.

Rutagwelela alisema wameshapata mkandarasi kwa ajili ya kazi hiyo na kwamba, wana uwezo wa kutosheleza mahitaji ya soko la ndani.

“Tumepokea rai ya naibu waziri, tunakwenda kuongeza uzalishaji. Zaidi ya tani bilioni tano za makaa ya mawe ziko chini ya ardhi kwenye Bonde la Mto Songwe, kwa hiyo wazalishaji wa saruji wasiwe na wasiwasi,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema migodi ya makaa ya mawe inayomilikiwa na Stamico ina barabara nzuri, hivyo aliwatoa hofu wazalishaji kuhusu changamoto ya usafirishaji wa malighafi.

Chanzo: mwananchi.co.tz