Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana wa Kamati ya Asasi za Kiraia Zanzibar (Zangof), imeandaa Mkutano wa Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kuangalia namna ya kushirikiana pamoja kuimarisha maedeleo ya na uchumi wa taifa hilo.
Majadiliano hayo ya siku tatu ambayo yanatarajiwa kufunguliwa kesho Mei 20, 2023 na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi, yakikutanisha asasi za kiraia na mashirika ya umma zaidi ya 250, yatashajiishwa na yenye kauli mbiu isemayo, ‘Kuimarisha mashirikiano baina ya asasi za kiraia na serikali kwa maendeleo ya Zanzibar.’
Mwenyekiti wa Zangof, Hassan Juma amesema ushirikiano huo utajengeka zaidi kwenye mipango ya Serikali ambapo pamoja na mambo mengne, utakujikita kuimarisha na kukuza uchumi wa buluu, uwajibikaji na matumzi sahihi ya rasimali za nchi.
“Mkutano wetu pia utajikita kujenga uelewa kuhusu michango ya asasi za kiraia, kuimarisha utawala bora na kuweka mikakati ambayo itasaidia mipango na vipaumbele vya kitaifa na kuainisha changamoto zao,” amesema.
Pamoja na hayo pia kutakuwapo na maonyesho ya kazi za taasisi mbalimbali ili kutoa uelewa kwa wadau kujua kazi muhimu ambazo wanatekeleza katika kuimarisha uchumi wa visiwa hivyo.
Amesema kutakuwa na mada ikiwemo mageuzi ya kisheria hususani majukumu ya taasisi za kisheria katika kuainisha sera na sheria.
Mratibu wa mkutano huo, Mahfoudh Shaaban amesema pamoja na mambo yote yanayotegemewa kufanywa ndani ya siku hizo mbili kuanzia Mei 20 hadi 22 pia zimeandaliwa tuzo 10 zitakazotolewa kwa asasi ambazo shughuli zake zimeonekana kufanya vyema katika kuchangia maendeleo na uchumi wa Zanzibar.
“Tuzo zinaangalia ni kwa namna gani miradi ya asasi hizo imeweza kuleta matokeo chanya na kujihusisha na jamii katika maendeleo visiwani hapa,” amesema.
Tuzo hizo zitatolewa kwa kwa asasi ambazo zimeonekana kufanya vyema katika vipengele ambavyo ni pamoja na afya, mazingira, uongozi na vijana.
Mjumbe wa Zangof, Shadida Omar amesema washiriki pia watapata fursa kujadili kwa kina maeneo muhimu ya utekelezaji na kutoa ushauri kwa serikali ili kuleta ufanisi.