Ikiwa imepita wiki moja tangu Katibu mkuu wa CCM, Daniel Chongolo kuagiza kiwanda cha chai cha Mponde wilayani Lushoto, Serikali imeanza mikakati ya utekelezaji wa agizo hilo.
Chongolo alitoa agizo hilo alipofanya ziara wilayani humo na kupata malalamiko kutoka kwa wakulima wa chai kukosa soko la zao hilo.
Jana Agosti 17 Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Joyce Ndalichako amekitembelea kiwanda hicho kilicho katika jimbo la Bumbuli na kueleza kuridhishwa na hatua za ukarabati wake.
Waziri amebainisha kwamba kiwanda hicho ambacho kimefikia asilimia 95 kukamilika na kuanza kazi mwishoni mwa mwezi Septemba, ili wakulima waanze kuuza majani ghafi ya chai kama awali.
Ndalichako amesema Serikali imewekeza Sh9 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa mitambo, miundombinu ya kiwanda pamoja na majengo ili yarudi katika hali yake ya kawaida baada ya uchakavu.
"Serikali imedhamira kufufua kiwanda hiki na ndio maana imetoa fedha hizo, kukikarabati kirudi katika hali yake ya kawaida ili kianze kazi mwishoni mwa Septemba.
“Katika Sh9 bilioni zilizotolewa na Serikali, Sh4 bilioni zimetumika kwa ajili ya ukarabati huu unaoendelea na Sh5 bilioni tano zilizobaki zitasaidia kuanzia mtaji wa kulipa watakaouza majani ya chai".
Amesema serikali imejiridhisha kwamba kiwanda kipo tayari kuanza kazi mwishoni mwa mwezi wa tisa baada ya kukamilisha uwekaji wa mambomba ya kukaushia chai ambayo ameagiza kazi hiyo iharakishwe haraka ili kiwanda kiweze kukanza kazi kama ilivyopangwa.
Nao baadhi ya wananchi waliozungumza katika mkutano wa Waziri Ndalichako, wameiomba Serikali itazame upya bei ya ununuzi wa majani ghafi ya chai ili iweze kulingana na gharama za uzalishaji kulikosababisha na kupanda kwa pembejeo.
"Bei ya kilo moja kwa sasa ni shilingi 314 hii bei ni ndogo tunaomba angalau ifike kati ya shilingi 700 hadi 1000 ili iendane na gharama za uendeshaji maana sasa hivi pembejeo bei sio kama ya zamani," amesema mmoja ya wakulima hao.
Naye Mwenyekiti wa Halmshauri hiyo Amir Shehiza amesema kufunguliwa kwa kiwanda hicho kutaongeza mapato yaliyopotea kwa muda mrefu.
"Kufungwa kwa kiwanda hiki kumechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa mapato ya halmashauri kwa kwakuwa kilikuwa chanzo kikuu cha mapato, kwa hiyo kikifunguliwa tunaimani hatutakuwa wa mwisho tena katika ukusanyaji wa mapato,” mebainisha.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kutoa ajira kwa wafanyakazi 70 wa kudumu kitakapo anza kazi na wengine 200 watakuwa ni vibarua.
Kiwanda hicho kiliingia mgogoro baina ya wawekezaji wa mwanzo na wakulima wa kilichokuwa chama cha ushirika wa wakulima wa chai wa Usambara Mashariki (Utega) hadi kupelekea kufungwa mwaka 2013.
Athari zilijotokeza baada ya kufungwa kiwanda hicho ikiwemo halmashauri kukosa mapato pamoja na kuyumba kwa uchumi wa wakulima hao.