Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali mbioni kuanzisha chombo kusimamia utalii wa fukwe

11393 Utalii+pic TanzaniaWeb

Sat, 14 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imesema ipo mbioni kutunga sheria itakayoanzisha chombo maalum cha kusimamia utalii wa fukwe nchini.

Chombo hicho kitakachofahamika kama Mamlaka ya Usimamizi wa Fukwe kitakuwa na jukumu la kuhakikisha fukwe zinakuwa kivutio cha utalii na kuliingiza Taifa fedha.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Julai 13, 2018 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla  alipokuwa akijibu swali kuhusu mikakati ya Serikali katika kukuza utalii wa fukwe.

Amesema pamoja na kuratibu shughuli zote kuhusu utalii wa fukwe, mamlaka hiyo pia itakuwa na eneo litakalotengwa maalum kwa ajili ya utalii huo.

"Eneo hili litatengwa maalum kwa ajili ya kuwavutia wawezaji kuwekeza kwenye aina hii ya utalii inayofanya vizuri Zanzibar,” amesema.

Kwa mujibu wa waziri huyo,  hatua kadhaa zimeendelea kuchukuliwa kuhakikisha vivutio vya utalii vilivyopo nchini vinatangazwa na kuleta matokeo chanya.

Amesema miongoni mwa jitihada zinazofanywa na Serikali katika kukuza utalii ni kuanzisha tamasha la urithi.

Amesema hatua ya kuanzishwa kwa tamasha hilo litakalofanyika Septemba kila mwaka,  inakwenda sambamba na juhudi za Serikali za kuongeza wigo wa mazao ya utalii nchini.

"Tamasha hili litafanyika kwa mwezi mzima kuanzia Septemba Mosi  tukiamini kuwa litasaidia kukuza utalii wa ndani na kuongeza wastani wa watalii wa kimataifa kukaa nchini. Hali hii itachangia kuongezeka kwa mapato,” amesema.

Tamasha hilo litaanza Septemba Mosi katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma likihusisha maonyesho ya ubunifu wa sanaa na utamaduni, vyakula,  kazi za wajasiriamali, burudani za ngoma za asili, muziki wa dansi na kizazi kipya.

Tamasha hilo litazinduliwa  Septemba 8 na Rais John Magufuli  na kumalizika  Septemba 29 ambapo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan atahudhuria.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz