Serikali ya Tanzania imeweka mikakati ya kuwasaidia wakulima wa zao la parachichi ikiwemo kujenga vituo vya masoko nchini.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Februari 3, 2022 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe katika kipindi cha maswali na majibu.
Bashe amesema Wizara imejipanga kuwasaidia wakulima wa zao hilo ikiwemo kuwapatia mbegu za ruzuku kwa lengo la kupungua gharama za uzalishaji.
Bashe amesema Serikali itajenga vituo katika mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam, Iringa na Songwe ambavyo vitawawezesha wakulima kulifikia soko kwa urahisi.
Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde amesema Serikali inaandaa mipango ya kuwasaidia wakulima wa zao hilo katika mikoa ya Songwe, Njombe, Mbeya na Iringa.
Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde akijibu maswali ya wabunge wakati wa kikao cha tatu cha mkutano wa sita wa Bunge, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi
Mavunde amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha zao la parachichi linalolimwa nchini Tanzania linakuwa na ubora unaokubarika duniani na kutambulika linapopatikana.
Swali la maboresho ya zao la parachichi limeulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee na Mbunge wa Makete Festo Sanga ambao wamehoji mkakati wa Serikali katika kuwezesha kilimo cha parachichi kiwe na tija.