Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuyapiga chini mashirika goigoi

09c5550a9407fe166344c6620334361b Serikali kuyapiga chini mashirika goigoi

Fri, 1 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imeshauriwa mambo kadhaa ya kuzingatia kabla ya kuyafuta mashirika ya umma yanayoonekana kuwa mzigo kwake na kwa umma.

Juzi wakati akipokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Rais Samia Suluhu Hassan alisema kuna mashirika yanayotumia fedha za serikali (fedha za uendeshaji) kulipana mambo makubwa makubwa, lakini hayana tija kwa taifa.

Kutokana na hali hiyo, alisema anadhani taasisi zinazohusika zikiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, wakae na kuyaangalia mashirika hayo kwa umakini na yale yanayotakiwa kufutwa yafutwe na yale ya kuimarisha yaimarishwe.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi waliohojiwa na gazeti hili wamesema watendaji waliopewa maagizo hayo wanatakiwa kutulia na kufanya kazi kitaalamu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Demokrasia na Utawala Bora Afrika (ForDIA), Bubelwa Kaiza, alisema ni vyema kauli ya Rais Samia ikafanyiwa kazi kitaalamu kwanza kabla ya kuanza kutekelezwa.

Kaiza alisema Tanzania ilikuwa na mashirika mengi, lakini serikali ilipoamua kuyabinafsisha mwaka 1995 hadi 2005, mashirika mengi yalikufa na watu walikosa kazi na baadhi ya waliouziwa hawakufanya chochote.

“Kama kuna suala ambalo linaonekana lina tatizo, liangaliwe kitaalamu na lishirikishe wafanyakazi wenyewe na wadau wengine kabla ya kufikiri kufuta shirika lolote,” alisema Kaiza.

Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Humphrey Moshi alisema mashirika ya umma yasipofanya kazi kwa ufanisi yanakuwa mzigo kwa serikali japo kuna mashirika ya umma ambayo ni lazima kuwepo.

Alisema kabla ya serikali kufikia hatua ya kuyafuta mashirika hayo, hainabudi kuangalia ni kitu gani kimesababisha yasifanye kazi kwa ufanisi.

“Wakati mwingine hayafanyi kwa ufanisi kwa sababu ya ukiritimba, mahali pengine hayafanyi kwa ufanisi kwa sababu serikali haitoi mtaji wa kutosha kufanya kazi, kwa hiyo lazima uangalie kwanza kitu gani kimesababisha shirika hilo lisifanye kwa ufanisi,” alisema Profesa Moshi.

Profesa Moshi alisema japo watu husema kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya maendeleo, lakini sekta ya umma ndiyo magurudumu ya hiyo injini.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, alisema kwa kuwa mashirika hayo yaliundwa kwa malengo mahususi yenye maslahi kwa Taifa, kuna haja kwa serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha kutokufanya vizuri kabla ya kufikia hatua ya kuyafuta.

Sakaya alisema kila shirika ambalo serikali ililianzisha lilikuwa na kusudi lake kwa maslahi ya taifa na mashirika hayo wamekabidhiwa watu wa kuyasimamia na kuyaendesha ambao walikuwa na matarajio waliyotaka kuyafikia ikiwemo kusaidia kuendesha uchumi na kutoa ajira kwa watu.

“Kwa hiyo mimi nadhani kabla ya kufikia hatua ya kuyafuta, kwanza yafanyiwe uchunguzi wa kutosha kubaini chanzo cha kuzorota kwake na uchunguzi huo uende sambamba na kuangalia menejimenti nzima ili kujua katika malengo waliyopewa wamekwama wapi, kwa sababu shirika haliharibiwi na watu wote, anaweza akawa mtu mmoja tu akafanya shirika lionekane halifai,” alisema Sakaya.

Aliongeza: “Kama ni mtu ndiye aliyesababisha washughulike naye, au kama ni idara fulani washughulike na idara hiyo, kama ni kitu kingine washughulike na hicho kitu kilichowafanya wakwame, hapa watakuwa wamepata taarifa nzuri itakayowasaidia na hatua ya kuyafunga iwe ya mwisho kabisa.”

Wakili wa Kujitegemea, Reuben Simwanza, alisema kabla ya serikali kufuta mashirika hayo, ni vyema ikazingatia sababu ya kuanzishwa kwake na utaratibu uliotumika kuyaanzisha.

Simwanza alisema kama kulikuwa na tija na muswada ukapitishwa wa kuyaanzisha kisheria, hivyo kuna haja ya kurudi na kuangalia mambo yaliyosababisha ikatungwa sheria ya kuyaanzisha.

“Lakini kama ikionekana, ile tija iliyosababisha kutungwa sheria na kuyaanzisha hayo mashirika haipo tena, ni sahihi sasa kupeleka tena muswada au hoja bungeni ya kuonesha kuwa kwa sasa mashirika haya ni ‘redundant’ (hayahitajiki) ili mabadiliko ya sheria yafanyike kuyaondoa,” alisema Simwanza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live