Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuwekeza sekta ya mawasiliano

Minara Mawasiliano Serikali kuwekeza sekta ya mawasiliano

Tue, 25 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesema itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuongeza mitaji na wawekezaji katika sekta ya mawasiliano kuinua uchumi wa nchi.

Aidha, imesema imekusudia kuipeleka Tanzania kidijitali na wadau wa mawasiliano ni muhimu katika kutimiza lengo hilo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema hayo wakati alipotembelea kampuni za simu za Tigo, Vodacom na Airtel jijini Dar es Salaam jana. Alisema wizara hiyo ipo tayari kutengeneza mazingira mazuri ya kushirikiana na wadau wa mawasiliano hata kama ni kupitia upya sheria zilizopo, sera, taratibu na namna ya kufanya kazi na wadau hao ili mwisho wa siku serikali iweze kutimiza wajibu wake wa kuwahudumia wananchi.

Alisema ametembelea kampuni za simu kwa sababu ni wadau muhimu kwani inakadiriwa kuwa karibu laini za simu milioni 55 zinatumika nchi nzima ilhali idadi ya Watanzania ni takribani milioni 60.

“Ukikuta laini za simu ni milioni 55 maana yake hizi kampuni zinagusa watu wengi lakini mchango wa sekta katika uchumi wa nchi ni mkubwa, wamewekeza fedha nyingi, wanalipa kodi na kuajiri Watanzania wengi,” alisema Nape.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Tigo Tanzania, Innocent Rwetabura alisema wako tayari kufanya kazi na serikali ili kuipeleka sekta ya mawasiliano mbele.

“Mwaka jana tulilipa kodi Sh bilioni 370, Sh bilioni 325 zikilipwa TRA na Sh bilioni 44 kwenye taasisi nyingine mbalimbali,” alisema.

Alisema Tigo Tanzania imeajiri wafanyakazi 1,233, pia ina mawakala zaidi ya 220,000 nchi nzima. Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Singano alisema wanaendelea kutoa huduma nafuu kwa nchi nzima ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Sitho Mdlalose alisema wanaendelea kuweka uwekezaji ili ifikapo 2025 wawe wamefikia Watanzania asilimia 80.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live