Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuwaendeleza wabunifu kibiashara

NDALICHAKO BUNGENI.webp Serikali kuwaendeleza wabunifu kibiashara

Sat, 20 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SERIKALI imetenga Sh. milioni 750 kwa ajili ya kuwaendeleza washindi 70 wa mashindano ya kitaifa ya sayansi, teknolojia na ubunifu (MAKISATU) ili kufanya ubunifu wao kuwa wa kibiashara.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini hapa, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, alipokuwa akitangaza washindi wa mashindano hayo kwa mwaka 2020.

Alisema fedha hizo zitatumika kuwaendeleza wabunifu hao ili kazi zao ziwe kibiashara na kuwainua kiuchumi.

Pia alisema serikali itaendelea kutenga fedha zaidi mwaka hadi mwaka kwa ajili ya kuendeleza ubunifu nchini.

“Natoa rai kwenu na washindi wote kuendeleza bunifu zenu ili kuhakikisha zinakuwa fursa za kiuchumi kwenu,” alisema Prof. Ndalichako.

Kadhali alisema serikali imetoa shilingi milioni tano kwa washindi wa kwanza kwa makundi yote, Shilingi milioni tatu kwa washindi wa pili na Shilingi milioni mbili kwa washindi wa tatu.

“Makundi yaliyoshiriki katika mshindano haya ni pamoja na shule za msingi, sekondari, vyuo vya ufundi stadi, vyuo vya ufundi wa kati, vyuo vikuu, taasisi za utafiti na maendeleo pamoja na mfumo usio rasmi,” alisema.

Alisema mashindano hayo hufanyika kila mwaka na kutoa fursa kwa wabunifu kujitangaza kwa wadau na watumiaji wa ubunifu na teknolojia zao.

“Mshindano yaliyopita tulianzia sekondari baadaye tulifanya tathmini na kubaini tunakosa kuibua vipaji vya watoto wadogo ndio maana tukaanzia kwenye shule za msingi na makundi mengine hadi vyuo vikuu,” alisema.

Vile vile, alisema kumekuwapo na ongezeko la washiriki na kwa mwaka huu walishiriki wabunifu 651 ikilinganishwa na mwaka 2019 walikuwa 415

Chanzo: www.tanzaniaweb.live