Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuvuna bil 50/- mkongo wa taifa

Ff2dec00e43b3d173551eb56f6d3cefa.jpeg Serikali kuvuna bil 50/- mkongo wa taifa

Thu, 20 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inakadiria kukusanya Sh bilioni 50 kutokana na mauzo ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo bungeni Dodoma jana, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile alisema wizara itaendelea na ujenzi wa mkongo huo uweze kufika maeneo ya wilayani jumla ya kilomita 1,880.

"Katika kujenga mkongo huo, ofisi za Halmashauri 17 pamoja na taasisi nyingine zitaunganishwa na miundombinu ya mtandao wa kasi na kupanua uwezo wa mkongo kutoka gigabit 200 (200G) hadi gigabit 400 (400G)," alisema Dk Ndugulile.

Alisema mradi huo utajumuisha ujenzi wa vituo vipya 17 vya kutolea huduma za mkongo ili kusogeza wigo wa utoaji wa huduma zake hadi ngazi za wilaya.

Dk Ndugulile alisema wizara hiyo pia inakusudia kutumia Sh bilioni 45 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Anwani za Makazi na Postikodi katika halmashauri 17 zikiwamo za Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza, Dodoma na Mbeya pamoja na manispaa za Kinondoni, Kigamboni, Temeke, Ubungo, Bukoba, Mtwara Mikindani, Tabora, Morogoro, Halmashauri ya Mjini Magharibi "B", Chakechake na Wete.

"Shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na kuweka miundombinu ya mfumo wa anwani za makazi na postikodi, kukusanya taarifa za barabara, nyumba na mitaa na kutengeneza na kuhuisha ramani za maeneo," alisema.

Alisema mwaka wa fedha 2021/22, taasisi zilizo chini ya wizara hiyo zinakadiria kukusanya Sh bilioni 424 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.

Chanzo: www.habarileo.co.tz