Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kuuza korosho ghafi, zilizobanguliwa

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imekaribisha wafanyabiashara mbalimbali kununua korosho ghafi na zilizobanguliwa.

Korosho zitakazouzwa ni tani 220,000 ambazo ni ghafi na tani 240 zilizobanguliwa.

Tangazo la TanTrade lililosainiwa na mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha mamlaka hiyo, Theresa Chilambo linaeleza kuwa wanunuzi wanaotakiwa ni wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda, hoteli, maduka ya jumla na rejareja, Supermarket, taasisi za umma na binafsi, vyuo, shule na wananchi.

Uuzwaji wa korosho hizo unakuja ikiwa ni siku chache tangu Rais John Magufuli alipofanya ziara mkoani Mtwara ambako pamoja na mambo mengine, aliitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kuuza korosho hizo kwa kuwa kadri zinavyokaa Serikali inatumia gharama kubwa kuzihudumia.

“Wizara ya viwanda imenunua mikorosho imekaa nayo inaiangalia mpaka ikutwe na ya mwaka huu?” Alihoji Rais Magufuli wakati akizindua kiwanda cha kubangua korosho cha Yalini mkoani Mtwara.

Akizungumza na gazeti la The Citizen, mkurugenzi mtendaji wa Tan Trade, Edwin Rutegaruka alisema: “Huu ni utaratibu wetu wa kawaida hatutangazi mauzo ya korosho tu bali tunafanya hivyo hata kwa mazao mengine, kwa sasa tayari tuna mazungumzo na baadhi watu walioonyesha nia ya kununua zao hilo.”

Alisema ni jukumu lao kutafuta masoko ya bidhaa za kilimo na nyinginezo zinazozalishwa nchini na bei ya korosho hizo itategemea na kiasi ambacho mnunuzi atahitaji.

Aidha Januari Kampuni kutoka nchini Kenya (Indo Power Solutions) iliingia makubaliano na Serikali kununua tani 100,000 za korosho kwa gharama ya Sh418 bilioni lakini biashara hiyo inaonekana kushindikana kwani kiasi hicho cha korosho kinachouzwa ni sehemu ya tani 221,000 ambazo zimekusanywa kwa msimu huu.

Kampuni ambayo vyombo vya habari vya Kenya viliripoti kuwa haina uwezo wa uwezo wa kufanya biashara hiyo ya mabilioni ya shilingi ilikuwa imekubaliwa kununua korosho hizo kwa bei ya Sh3,300 sawa na bei ambayo Serikali ilinunulia kutoka kwa wakulima.



Chanzo: mwananchi.co.tz