Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kutoa Sh2 billioni kutatua tatizo la maji Kiabakari

12734 KIABAKARIIII TanzaniaWeb

Mon, 20 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Musoma. Serikali imeahidi kutafuta fedha za dharura zaidi ya Sh2 bilioni za kukarabati kilomita saba za miundombinu ya maji katika mradi wa maji wa Mugango-Butiama ili kuwawezeshia huduma wakazi wa Kijiji cha Kiabakari wilayani Butiama kupata maji.

Ahadi hiyo imetolewa leo Agosti 19 na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa alipozungumza na wakazi wa kijijini hicho katika ziara yake mkoani Mara ya kutembelea na kukagua miradi iliyo chini ya wizara yake.

"Kuharibika kwa miundombinu hii kunasababisha upotevu wa maji na kuwakosesha huduma wananchi; tutaitafutia ufumbuzi wa dharura kwa kuufanyia ukarabati kusubiri mradi mkubwa wa maji utakaomaliza kabisa tatizo la ukosefu wa maji katika wilaya za Musoma na Butiama," amesema Mbarawa.

Miundombinu ya maji katika mradi huo unaotegemewa na wakazi wa Kiabakari una urefu wa kilomita 19 ambaza saba zimeharibika na kusababisha upotevu wa maji njiani.

Awali, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walimweleza Waziri Mbarawa kuwa tatizo la maji kijijini hapo linakwamisha maendeleo yao kiuchumi kwa sababu wanalazimika kutumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo badala ya kushiriki shughuli za uzalishaji mali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Waziri na msafara wake, Sabina  Marwa na Isaac Jackson wameiomba Serikali kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya kumtwaa mama ndoo kichwani kwa kuhakikisha kijiji hicho kilicho umbali wa kilomita tisa pekee kutoka chanzo cha maji kinapata huduma ya uhakika.

"Wakati mwingine kijiji chetu kinapata huduma ya maji ya bomba mara moja kwa mwezi licha kuwa kilomita tisa tu kutoka kwenye chanzo," Jackson amemweleza Waziri.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz