Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewaagiza Naibu Katibu Mkuu, Sekta ya Mifugo, Profesa Daniel Mushi na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyopo katika Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco) mkoani Kagera ambayo hayana mgogoro yatangazwe kwa ajili ya uwekezaji.
Ulega ametoa maelekezo hayo, leo Januari 22, 2024 kwenye kikao kati yake na viongozi wa Mkoa wa Kagera kilicholenga kumaliza migogoro iliyopo baina ya wananchi na ranchi za Taifa.
Amesema maeneo ambayo yameshapimwa na yasiyo na mgogoro yatangazwe ili wawekezaji wenye uwezo wapewe kwa ajili ya kufanya ufugaji wenye tija.
Pia amewataka wataalamu kurejea upya kwenye maeneo yote ambayo yameonekana yana migogoro ili kutatua changamoto zilizopo na kuwezesha maeneo hayo yaendelezwe na wawekezaji wenye uwezo.