Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali kusitisha vibali viwanda kuagiza sukari

9aa2266ab4477b357cd14ab9176671fe Serikali kusitisha vibali viwanda kuagiza sukari

Tue, 16 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Kilimo, imesema ifikapo mwaka 2022 serikali haitatoa vibali kwa kampuni zinazozalisha sukari kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi badala yake wanatakiwa waongeze uchakataji wa miwa ya wakulima na zizalishe sukari ya kutosha mahitaji ya ndani.

Waziri wa wizara hiyo, Profesa Adof Mkenda, jana alisema, utaratibu wa sasa wa viwanda kupewa vibali vya kuagiza sukari nje hauna manufaa kwa taifa.

Alitoa msimamo huo wakati akizungumza na uongozi wa mkoa wa Morogoro akiwa ziarani kukagua hali ya uzalishaji sukari katika viwanda vilivyopo mkoani humo.

Alisema, ni lazima katika mipango yao washirikiane na wakulima wa miwa ili malengo ya kitaifa yafanikiwe.na kuwa serikali inafuatilia kwa karibu utendaji kazi wa viwanda vya kuchakata sukari nchini.

"Shida yetu ya sukari haitokani na kukosa miwa bali ni uwezo mdogo wa viwanda kuchakata miwa yote ya wakulima nchini hali inayosababisha baadhi ya miwa ya wakulima kukosa soko" alisema Waziri Mkenda.

Prof Mkenda alibainisha kuwa wizara ya kilimo ina mkakati wa kuhakikisha miwa yote ya wakulima inachakatwa na viwanda vilivyopo ili kuondoa tatizo la upungufu wa sukari na kuwa utaratibu wa sasa viwanda kupewa vibali vya kuagiza sukari nje hauna manufaa kwa taifa.

Ili kuwa na uhakika wa sukari Prof. Mkenda amesema wizara inahamasisha matumizi ya mbegu bora na kilimo cha umwagiliaji pamoja na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vipya vya sukari.

"Mwaka huu vibali vya kuagiza sukari itakayopungua itatolewa kwa makampuni kwa utaratibu wa kawaida lakini ifikapo mwaka 2022 hakutakuwa na vibali vya viwanda na ikilazimu basi Bodi ya Sukari ndio itapewa kibali cha kuagiza sukari itakayopungua " alisisitiza Prof Mkenda

Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Emanuel Kalobero, alisema mkoa huo una viwanda vitatu vya kuzalisha sukari ambavyo bado uzalishaji wake ni mdogo hivyo kusababisha miwa ya wakulima ikose soko na kuharibika.

Alitaja viwanda hivyo na uzalishaji wake kwenye mabano kuwa ni Kilombero Sugar Ltd I na Kilombero Sugar II kwa pamoja huzalisha (tani 126,000) na kiwanda cha Mtibwa (tani 50,000) huku uzalishaji wa miwa kwenye bonde la Kilombero unaofanywa na wakulima wadogo umefikia wastani wa tani 800,000 hadi 1,000,000 na uwezo wa kiwanda cha Kilombero ni kuchakata tani 600,000 tu za wakulima wadogo kwa mwaka.

"Mfano uzalishaji wa miwa ya wakulima wadogo ni kati ya tani 800,000 hadi 1,000 000 na uwezo wa kiwanda ni tani 600,000 " alisema Kalobero.

Kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya Sukari Tanzania uzalishaji wa sukari kwa mwaka ni takribani tani 300,000 na kwa mwaka 2020/21 ulifikia tani 377,527 na mahitaji ya sukari kwa matumizi ya kawaida na viwandani ni tani 655,000

Viwanda vinavyozalisha sukari nchini ni pamoja na Kilombero, Mtibwa, Kagera, TPC na Manyara.

Chanzo: habarileo.co.tz